Seth, Rugemalira wafikisha mwaka na miezi sita rumande

Muktasari:

Kutokana na upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi  inayowakabili Habinder Seth na James Rugemalira kutokamilika shauri hilo limeahirishwa hadi Desemba 20, 2018 na kuwafanya watimie mwaka mmoja na nusu wakiwa mahabusu

Dar es Salaam. Washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi, Habinder Seth na James Rugemalira  wanaendelea kusota rumande kwa takribani mwaka moja na miezi sita sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 19, 2017  kujibu mashtaka  12 yakiwemo ya utakatishaji fedha lakini hadi sasa  upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Rugemalira ambaye  ni  mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Seth ambaye ni mwenyekiti mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.

Leo Alhamisi Desemba 6, 2018 upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili wa Takukuru,  Leonard Swai amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Huruma Shaidi kuwa  kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 20, 2018.

Seth na Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka  12 ya uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika shtaka la kwanza  washtakiwa wanadaiwa kuwa  kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma  walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la tatu, Seth anadaiwa kuwa Oktoba 10,2011 katika mtaa wa Ohio Ilala jijini Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14  ya usajili wa kampuni  na kuonesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.