Sh100 inavyomkumbusha baba mtoto wake aliyeuawa muuaji akitaka Sh10 milioni

Muktasari:

  • Ni mtoto aliyetekwa Mbeya na mtekaji kudai apewe Sh10 milioni ili amuachie akiwa hai, alipoona mambo hayamwendei sawa aliamua kumuua na kumtupa shambani.

Baba wa mtoto Junior Siame (8) ambaye aliuawa kwa kunyongwa baada ya kutekwa na kijana mmoja anayeshikiliwa na polisi Jijini Mbeya, Bakari Siame amesema kitendo cha mwanaye kutekwa na kunyongwa ni kidonda ndani ya maisha yake ambacho hakitapona kamwe.

Aprili 9, mwaka huu, mtoto Junior alitekwa na mtu ambaye hakufahamika kabla ya kunyongwa kisha mwili wake kutelekezwa Mlima Nyoka karibu na mashamba ya mahindi nje kidogo ya Jiji la Mbeya.

Kabla ya mtekaji huyo kutekeleza mauaji hayo alimpigia simu baba mzazi wa mtoto huyo na kumwambia yupo na mwanaye na ili amuachie akiwa hai amtumie Sh10 milioni.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Mtaa wa Sai Jijini Mbeya, Siame alisema hadi sasa anashindwa kuamini kama amempoteza mtoto wake kipenzi ambaye alikuwa akizunguka naye sehemu mbalimbali baada ya kutoka shuleni na siku za mapumziko.

“Nimeumia kumpoteza kijana wangu, kipenzi changu ambaye nilikuwa nampenda tuliyekuwa tunataniana kama mtu na mdogo wake kwani kila akirudi kutoka shuleni alikuwa haniiti baba aliniita ‘Mose’ naomba Sh100 ya kula shuleni.

Hata hivyo sina namna nyingine…namuombea kwa Mungu amuweke mahali pema peponi,” anasimulia Bakari huku akibubujikwa na machozi.

Bakari anasema kitu ambacho kinamuumiza ni pale anapokumbuka alivyokuwa akizunguka naye maeneo mbalimbali kama vile kwenye vibanda vya kuangalia mpira, saluni alikokuwa akimpeleka kunyoa nywele na muda mwingine alikuwa akiongozana naye hadi Uwanja wa Sokoine kunapokuwa na mechi.

Anasema “nikikumbuka wakati nazunguka naye kila sehemu kama katika vibanda vya kungalia mpira na saluni kwenda kunyoa. Ilikuwa nikinyoa naye ananyoa, tulikuwa kama mapacha…ingawa kanitoka machoni lakini hawezi kunitoka moyoni, nilikuwa nampenda mwanangu”.

Anasema mtoto wake alikuwa na juhudi ya kujisomea pindi akirudi nyumbani kwani alikuwa na ndoto ya kufanya kazi benki au kuwa rubani.

“Mtihani nilionao sasa nafikiria nani atakuwa ananiita ‘Mose’ na ni nani atakuwa ananiomba Sh100 ya kula shuleni kila asubuhi anapokuwa ameamka kujiandaa kwenda shuleni. Naomba Serikali isimuachie kijana aliyehusika na mauaji ya mtoto wangu,” anasema.

Hata hivyo, Siame anasema pengo la kuondokewa na mtoto huyo halipo kwake tu bali hata kwa mke wake ambaye ni mjasiriamali ambaye anasema mpaka sasa hayuko sawa kisaikolojia. Junior alikuwa anamwagiza mama yake juisi, miwa na matunda jambo ambalo walijivunia.

“Nina watoto wawili kutoka kwa mama tofauti ambao ni wa kike na wa kiume ambaye ni Junior na ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa ila huyu mwingine sijamzoea kama marehemu kwa kuwa siishi naye, yeye anaishi na mama yake ingawa nampenda pia,” anasema.

Jinsi ilivyokuwa

Akisimulia tukio hilo, Siame anasema Jumanne ya Aprili 9, mwaka huu asubuhi mwanaye alikwenda shuleni na saa tisa mchana alirejea nyumbani kama kawaida.

Anasema saa 10 jioni alikwenda kwenye masomo ya jioni, ndipo akakutana na mtu asiyemjua kisha akamteka bila ya wao kujua na walisubiri hadi jioni muda ambao huwa anarudi nyumbani lakini hakuonekana hivyo wakashikwa na hofu.

Anasema baada ya kutorudi nyumbani hadi saa moja kasoro jioni, walikwenda kumuulizia kwa marafiki zake ambao walisema hawajamuona, wakarejea nyumbani na baadaye wakaenda kutoa taarifa kituo cha polisi.

“Hizi taarifa za kutekwa ni kwamba, jirani yetu fundi friji alikuja hapa ambaye mtekaji alikuwa akiwasiliana naye, na mtekaji akatuambia kwa njia ya simu kwamba mwanangu anaye huko na anahitaji Sh10 milioni taslimu ndipo amuachie,” alisema.

Anasema baada ya kuzungumza na mtekaji huyo alitoa taarifa polisi, na akaambiwa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kumnasa mtuhumiwa huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Oulrich Matei alisema baada ya kupata taarifa za kutekwa kwa Junior, kikosi kazi kilifanya kazi usiku na mchana kumtafuta na hatua ya kwanza wakapata mawasiliano ya mtekaji na baadaye wakabaini mtuhumiwa huyo yupo mkoani Iringa.

“Kikosi kiliendelea na jitihada zote hadi juzi (Ijumaa) wiki iliyopita kikosi kazi cha Mbeya kilikwenda Iringa, tukafanikiwa kumpata mtuhumiwa maeneo ya Ipogolo akiwa amejificha na alipokamatwa alieleza ndiye aliyeshiriki kwenye tukio la kumteka mtoto Junior na alikwenda jijini Mbeya akaonyesha mahali alipomuulia eneo la Mlima Nyoka karibu na mashamba ya mahindi,” alisema Kamanda Matei.

Anasema baada ya kumhoji alieleza kila kitu namna alivyofanikisha kumteka mtoto huyo.

Kamanda Matei alisema mtuhumiwa alimtumia jirani wa wazazi ambaye ni fundi friji kuwasiliana nao na kudai kiasi hicho cha fedha ili amuachie mtoto huyo akiwa hai. Hata hivyo, anasema baadaye aliondoka na Junior hadi eneo la Nsalaga alikomuua na kumtupa baada ya kuhofia mtoto huyo angepiga kelele na kusababisha atiwe mbaroni.