Mabilioni ya Deci yataifishwa

Dar es Salaam. Kama mtu alikuwa akisubiri fedha ‘alizopanda mbegu’ katika kampuni ya upatu ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci) ili ‘avune’ fedha nyingi zaidi, sasa hataambulia chochote.

Hali hiyo inatokana na amri ya Mahakama Kuu kuwa mali za kampuni hiyo zitaifishwe.

Uamuzi wa kutaifisha mali za Deci, ikiwa ni pamoja na magari, nyumba, viwanja pamoja na Sh14.1 bilioni zilizoko katika akaunti za kampuni hiyo katika benki mbalimbali jijini Dar es Salaam, ulitolewa jana na Jaji Stephen Magoiga.

Jaji Magoiga alifikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwa mali hizo zilitokana na mapato ya uhalifu, yaani kuendesha shughuli za upatu za kukusanya pesa kutoka kwa umma bila kuwa na leseni.

Jaji Magoiga alisema ameridhika na hoja na ushahidi wa DPP baada ya wakurugenzi wa Deci kushindwa kutoa ushahidi wa jinsi walivyozipata mali hizo, licha ya kupinga kwa maneno kwamba hazikutokana na Deci.

Jaji Magoiga alisema kwa kushindwa kutoa ushahidi wa kupinga mali hizo kutaifishwa, viongozi wa Deci wameshindwa kutimiza wajibu wao na matakwa ya kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Mali Zitokanazo na Uhalifu (Poca).

“DPP au Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) anapowasilisha mahakamani maombi ya kutaifishwa kwa mali za washtakiwa waliotiwa hatiani kwa uhalifu, mtu anayepinga maombi hayo anapaswa kuwasilisha mahakamani ushahidi kuwa mali hizo hazikutokana na uhalifu,” alisema Jaji Magoiga.

“Kwa kutokuwepo ushahidi huo wa kuonyesha kuwa mali hizo hazikupatikana kwa njia ya uhalifu na kuelezea source (chanzo) nyingine ya upatikanaji wa mali hizo, ninabaki tu kuzingatia ushahidi wa mwombaji.”

Alisema sheria hiyo inaelekeza kuwa katika maombi yao, DPP au AG anawajibika kutoa taarifa kwa mhusika wa mali hizo na kwa umma ili kama kuna mtu ambaye anapinga kuwa mali hizo si za uhalifu au ni zake, aweze kufika mahakamani na kutoa ushahidi huo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa jaji huyo, hakuna mtu aliyefika mahakamani kudai mali hizo zote au sehemu na kwamba wakurugenzi hao wa Deci, licha ya kupinga katika hati yao ya kiapo kinzani kuwa mali hizo si za uhalifu, hakuna hata aya moja inayoelezea jinsi walivyozipata.

Hivyo, Jaji Magoiga aliamuru mameneja wa matawi ya benki hizo ambayo yana akaunti za Deci kama vile NMB Msasani, Dar es Salaam Community Banki (DCB), tawi la Uhuru na Kenya Commercial Bank (KCB), Samora Avenue, Dar es Salaam wahakikishe wanapeleka fedha hizo serikalini.

Pia aliamuru nyumba na viwanja vibadilishwe usajili kutoka Deci na visajiliwe kwa jina la Msajili wa Hazina na maeneo ambayo hayajapimwa yapimwe na kusajiliwa kwa jina la Msajili wa Hazina.

Vilevile, Jaji Magoiga ameamuru DPP awasilishe mahakamani maombi ya kupata dalali wa mahakama kwa ajili ya kuwatoa watu wote wanaoishi katika nyumba hizo na kuzikabidhi kwa Serikali.

Amri nyingine ni kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kubadili umiliki wa magari hayo kutoka kwa Deci na kuwa mali ya Serikali.

Jaji Magoiga alibainisha kuwa lengo la kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu kwa mujibu wa sheria hiyo, siyo kutaka kuitajirisha Serikali, bali ni kutaka kuzuia watu wengine kujipatia mali kwa njia hizo za uhalifu.

DPP alifungua maombi hayo mwezi Machi mwaka huu, miaka takribani sita baada viongozi hao wa Deci kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2009, kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu kinyume cha sheria.

Viongozi wa Deci, ambao walikuwa wachungaji, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekosti, walitiwa hatiani kwa kosa hilo mwaka 2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni. Walilipa faini na hivyo wakaepuka kifungo.

Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye na Samwel Sifael Mtares.

Hata hivyo, wakili wao, Majura Magafu aliiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo akidai kuwa mwombaji ameshindwa kutoa ushahidi mahakamani kuthibitisha kuwa mali hizo zote zimetokana na makosa hayo yaliyowatia hatiani.

Alisema kuwa si kila anayetiwa hatiani kwa makosa kama hayo lazima mali zake zitaifishwe na kwamba Sheria ya Ushahidi kifungu cha 110 kiko wazi kwamba ni jukumu la kila anayeiomba mahakama imtendee analoliomba kuithibitishia mahakama kuwa anastahili hicho anachokiomba.

Awali Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema kuwa wajibu maombi hao walikubali katika utetezi wao kuwa Deci haikuwa na biashara nyingine isipokuwa kupokea amana za wanachama, lakini Wakili Magafu alisema kuwa walikubali kuwa mali nyingine zilikuwa zao binafsi na nyingine za Deci.

Alidai kuwa wana ushahidi wa kutosha kwamba mali walizoziorodhesha katika maombi hayo zikiwemo pesa hizo zimetokana na kosa hilo.

Wakili Kimaro alirejea ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa wajibu maombi hayo katika kesi ya msingi, ambao walidai kuwa Deci haikuwa na biashara nyingine zozote zaidi ya kupokea amana kutoka kwa wanachama.

Pia ziliwekwa kwenye akaunti ya kanisa kwa kuwa bado walikuwa katika mazungumzo pamoja, huku akirejea utetezi wa baadhi ya wajibu maombi kuwa hawakuwa na biashara nyingine zaidi ya upatu.

Mali zilizotaifishwa

Mali zilizotaifishwa ni pamoja na fedha hizo zilizoko katika akaunti na benki tofautitofauti kama vile Sh12.5bilioni zilizoko NMB, tawi la Msasani.

Nyingine ni Sh1.458 bilioni zilizoko Dar es Salaam Community Bank (DCB), tawi la Uhuru na Sh57.93 milioni zilizoko Kenya Commercial Bank (KCB), tawi la Samora.

Mbali na pesa hizo, mali nyingine za Deci ambazo mahakama iliombwa iamuru zitaifishwe ni pamoja na nyumba namba UKMMD/1237 iliyoko Mwembe Madafu, Ukonga, Dar es Salaam, kiwanja namba 651, kitalu “M” kilichopo Forest, Mbeya,

Nyumba nyingine ni ile iliyoko kiwanja namba 7, kitalu “P” Mtaa wa Rufiji, Manispaa ya Mwanza, nyingine iliyoko Mabibo, Kinondoni na ardhi ambayo haijapimwa.