Shabiby ashauri namna ya kuondoa foleni Dar

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby,

Muktasari:

  • Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, ameitaka Serikali kujenga bandari kavu eneo la Vigwaza ili kuondoa changamoto zinazosababishwa na uwapo wa malori mengi jijini Dar es Salaam na wakati mwingine kusababisha ajali kwa magari kudondokewa na makontena

Dodoma. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby ameitaka Serikali kujenga bandari kavu eneo la Vigwaza mkoani Pwani ili kuondoa msongamano wa malori yanayotoka katika bandari ya Dar es Salaam.

Shabiby ameyasema hayo leo Alhamis Mei 8 2019 akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na kwamba, wizi wote uliokuwa unajitokeza zamani hivi  sasa haupo.

“Mmoja wa watu ambaye nilikuwa situmii Bandari ya Dar es Salaam ni mimi lakini katika miaka mitatu sasa natumia na wakati mwingine nawategeshea vitu loose ili nione kama vitaibwa, lakini iko vizuri sana haina wizi na ina speed (kasi) ya hali ya juu sana,” amesema.

Hata hivyo, Shabiby amesema kutokana na uzuri huo kumeleta changamoto ya msongamano wa malori.

“Kwa sababu ya uzuri wa bandari hiyo kumekuwa na malori mengi yanayopita katika barabara zetu. Sasa tulizungumza sana tuanzishe dry port (bandari kavu) ya pale Vigwaza ili malori yawe yanaishia hapo na mizigo  ichukuliwe na reli ambayo sasa hayafanyi kazi hadi Vigwaza,” amesema.

Amesema malori yamezidisha foleni na kwamba, kujengwa kwa bandari   kavu kutasaidia kuondoa foleni kwa sababu malori hayataingia ndani ya   Dar es Salaam.

Amesema gharama ya kutoa mizigo bandarini kwa kutumia reli ni nafuu zaidi ya mizigo hiyo kubebwa na malori.

“Mfanye haraka zaidi ifanye kazi. Sasa inasababisha vifo mara kontena imeangukia Hiace,”amesema.

Pia, aliitaka Serikali kujenga barabara ya kati ya Kongwa na Mpwapwa ambayo ahadi ya ujenzi wake ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

“Huyu mbunge (Mbunge wa Mpwapwa George Lubeleje) mtamuua mzee hadi meno yameng’oka lakini hamsikilizi barabara ya Mpwapwa ni muhimu kuliko barabara nyingine za Mkoa wa Dodoma,” amesema.

Amesema wameangalia pamoja na Lubeleje, lakini haimo kwenye bajeti na kwamba iko katika ilani ila hakuna haina dalili hadi leo.