Shahidi adai kufanyiwa aina nane za mateso akiwa mikononi mwa polisi

Wananchi wakitoka katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi mkoani Kilimanjaro juzi baada ya kuhairishwa kwa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Serkondari Scolastica Iliyopo Himo, Humphrey Makundi. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Kesi hiyo ya mauaji inamkabili mmiliki wa Shule ya Scolastica, Edward Shayo, pamoja na mwalimu wa nidhamu, Laban Nabiswa na mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha.

Moshi. Shahidi wa utetezi, Hamis Chacha ameeleza mateso ya aina nane anayodai alifanyiwa na polisi ili kuandika maelezo ya kukiri kosa la mauaji ya mwanafunzi wa Shule ya Scolastica, Humphrey Makundi.

Alikuwa akitoa maelezo hayo katika kesi ndogo ndani ya kesi ya mauaji inayoendelea Mahakama Kuu.

Chacha alidai kuwa alipigwa kwa shoti ya umeme, kuunguzwa kwa pasi ya umeme, kuingiziwa sindano kwenye uume wake na kuingiziwa chupa ya bia sehemu ya haja kubwa.

Kesi hiyo ya mauaji inamkabili mmiliki wa Shule ya Scolastica, Edward Shayo, pamoja na mwalimu wa nidhamu, Laban Nabiswa na mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha.

Chacha ambaye alimaliza kutoa ushahidi wake saa 2:20 usiku mbele ya Jaji Firmin Matogolo, alitaja mateso mengine kuwa ni kupigwa kwa bakora, kulazwa uchi, kunyimwa chakula na kulazwa chumba chenye maji.

Chacha, ambaye alikuwa akiiongozwa na wakili David Shillatu, alidai kuwa Novemba 17, 2017 akiwa shuleni Scolastica, alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Himo akiwa na mlinzi mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Mchamungu na wakawekwa mahabusu.

Alidai ilipofika saa 2:00 usiku, walitolewa mahabusu na kupelekwa mapokezi ambako polisi mmoja alimpiga kwa bakora nyeusi na mwingine akimpiga kwa kitako cha bunduki.

Aliiambia mahakama kuwa muda huohuo walihamishiwa kituo cha kati ambako waliwekwa chumba kimoja, lakini baada ya muda alichukuliwa na kupelekwa eneo jiingine.

“Kwenye hicho chumba kulikuwa na pikipiki na redio ya subwoofer. Niliwakuta polisi watatu na yule aliyenichukua akawa wa nne. Niliambiwa nivue nguo zote nibaki kama nilivyozaliwa,” alieleza.

Akiwa hapo, anadai alifungwa pingu miguuni na mikononi kwenye meza na polisi walianza kumpiga kwa bakora, kabla ya kumfungua na kuweka chupa ya bia na kumlazimisha aikalie.

Shahidi huyo alidai wakati wakimtesa walimtaka akubaliane nao na aeleze kuwa Novemba 6, 2017 usiku wa saa 2:58 kuna mtu aliruka ukuta kutokea ndani ya shule na akamkurupusha kuelekea uraiani.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, alitakiwa kueleza kuwa baada ya kumkimbiza alimpiga na mabapa ya panga hadi akafariki dunia na ndipo alimpompigia simu Laban na mmiliki wa shule hiyo.

Pia, alitakiwa aseme kwamba baada ya mmiliki kufika hapo aliagiza wachukue mwili huo na kuutupa Mto Ghona kwa madai kuwa usiku ule ulikuwa haujatambulika.

Hata hivyo, alidai aligoma kusaini maelezo hayo, ndipo polisi walipoendelea kumtesa kwa umeme na kumuunguza kwa pasi ya umeme, hiyo ikamfanya akubali kusaini maelezo hayo.

Alieleza kuwa Novemba 19, 2017, polisi hao walimchukua na kumueleza kuwa kesho yake wangempeleka kwa mtu waliyemuita ni “bosi wao” (mlinzi wa amani) na aeleze kama alivyoandika.

Wakati anasita, alitokea mtu aliyemtaja kuwa ni Godvictor Munisi aliyekuwa na sindano ndefu, na aliingiza katika uume wake na kutokana na maumivu makali aliyopata, alikubali kufanya walichotaka.

Mbali na Munisi, aliwataja polisi aliodai walikuwa wakimfanyia ukatili huo kuwa ni Inspekta Waziri Tenga, Inspekta Fredy Kisanga, Inspekta Leons, na polisi wengine wawili ambao hawafahamu majina.

Novemba 20, 2017 alipelekwa kwa bosi huyo na alitoa maelezo kama alivyoelekezwa na baadaye mtu mmoja alimshurutisha kusaini maelezo yanayodaiwa ni ya ungamo na kuweka dole gumba.

Baada ya kutoa ushahidi huo, upande wa Serikali wakiongozwa na Joseph Pande, pamoja na Abdalah Chavulla, Omary Kibwana na Wakili Lucy Kyusa walimuhoji shahidi huyo:

Wakili Pande: Kama nilikuelewa, umesema ulipelekwa kwa mtu anaitwa Irene Mushi kuandika maelezo yako, ni kweli?

Shahidi: Nilipelekwa kwake huyo waliyesema ni bosi wao.

Wakili Pande: Kwamba Irene Mushi alikuwa anaandika kile ulichokuwa unamueleza

Shahidi: Ndio mheshimiwa

Wakili Pande: Hiyo nyaraka (maelezo ya ungamo) aliyokuwa anaiandika wewe ulipata fursa ya kuipitia, kuisani na kuweka dole gumba?

Shahidi: Ndio niliweka

Wakili Pande: Kuna mtu aliyekushurutisha uweke saini na dole gumba?

Shahidi: Simfahamu kwa jina ila ni mwanaume. Alishika kidole changu na kukandamiza

Wakili Pande: Na vile vile ukasaini bila ridhaa yako?

Shahidi: Yule bosi wake ndio alimuamuru kuwa Chacha asaini hapo.

Wakili Pande: Umesema hapa ulipigwapigwa, kipi ambacho kilitangulia, kipigo au kile walichokitaka?

Shahidi: Walianza na kipigo na baadaye mateso.

Wakili Pande: Lakini, ulivyofika kwa mlinzi wa amani ukamuonyesha alama za fimbo tu?

Shahidi: Kwa mila na desturi zetu sisi Wakurya hatuwezi kumvulia nguo mwanamke ambaye sio mke wako.

Wakili Pande: Tukubaliane kwamba yale ambayo Hakimu aliandika ni yale tu uliyoelekezwa na Inspekta Tenga, si ndio?

Shahidi: Ndio.

Wakili Pande: Hata suala la kusema ulipigwa na askari wengi ni Tenga alikuambia pia?

Shahidi: Hayakuwa maelekezo ya Tenga.

Wakili Pande: Inspekta Tenga alipokuwa anatoa ushahidi hapa asubuhi hukumuuliza swali lolote kwamba wamekuonea?

Shahidi: Ndio aliulizwa.

Wakili Pande: Kwamba aliulizwa wewe Tenga ndio ulimwelekeza Leons akuchome na pasi.

Shahidi: Hilo swali hakuulizwa

Wakili Pande: Irene alipokuwa anatoa ushahidi hapa aliulizwa wewe ndio uliomshurutisha Chacha aweke saini na dole gumba?

Shahidi: Hakuulizwa.

Wakili Chavulla: Uliiambia mahakama uliingiziwa chupa ya bia, ilikuwa na ukubwa gani?

Shahidi: Inaanza nyembamba (akionyesha) halafu inaongezeka unene.

Wakili Chavulla: Kwani ile chupa ilipakwa mafuta?

Shahidi: Haikuingia kwa raha bwana yalikuwa mateso.

Wakili Chavulla: Ilikuwa mara yako ya kwanza kuingiziwa kitu kigumu na bado una ujasiri wa kusimama na kutembea?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, hata mwanamke anafanyiwa na anatembea itakuwa mwanamme ashindwe kutembea?

Wakili Kibwana: Tarehe 6.11.2017 usiku (siku ya tukio la mauaji) ulimpigia simu Mzee Shayo na mwalimu Laban?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Kibwana: Ni kweli kwamba Mzee Shayo naye alikupigia usiku huo huo

Shahidi: Nilimpigia kweli hatukuelewana ndio akanipigia.

Wakili Kibwana: Ni kweli mwalimu Laban naye alikupigia usiku huo.

Shahidi: Alinipigia.

Wakili Kyusa: Ni kweli kwamba katika walinzi wanne wa Scolastica ni wewe tu umeshitakiwa?

Shahidi: Ndio.

Wakili Kyusa: Ni kweli kwamba tarehe 27.11.2017 ulifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa shitaka hili la mauaji?

Shahidi: Ndio na niliambiwa hakuna kujibu chochote.

Wakili Kyusa: Ni kweli hukuona umuhimu wa kumwambia Hakimu kuhusu mateso na vidonda ulivyovipata?

Shahidi: Niliambiwa hakuna kujibu chochote.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Jumatatu wakati Jaji Matogolo atakapotoa uamuzi mdogo wa kama maelezo ya ungamo ya mshitakiwa huyo, yapokelewe kama kielelezo cha kesi hiyo ama la.