Shahidi aeleza alivyochukizwa na polisi baada ya kumsikia Zitto

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa Jamii Media Max Mero katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Ni maelezo aliyoyatoa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya Zitto Kabwe anayetuhumiwa kutoa maneno ya uchochezo dhibi ya polisi

Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu namna alivyolichukia Jeshi la Polisi hadi leo, baada ya kusikia kwenye video iliyopo kwenye mtandao wa kijamii wa Youtube.

Mashaka Juma, ambaye ni msanii wa filamu amedai video hiyo ilikuwa ikimuonyesha Zitto Kabwe akielezea polisi walivyochukua watu hospitali kwenda kuwaua.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, leo Alhamisi, Mei 16, 2019, shahidi huyo amedai Oktoba 29, 2018 akiwa eneo la Kimara Korogwe na wenzake wanacheza drafti, alikuja mwenzao anaitwa Frenky Zongo.

Amedai alipofika aliwauliza kama wamepata habari yoyote, lakini walimweleza hawana, hivyo akawaeleza ‘Zitto ndio habari ya mjini’ na kutoa simu kisha akawafungulia Youtube waangalie.

Shahidi huyo ameeleza wakati wanaangalia walimuona Zitto akililaumu Jeshi la Polisi kwa mambo mbalimbali ambayo wameyafanya wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Amedai katika video hiyo, inamuonyesha Zitto akieleza namna Jeshi la Polisi likiwanyanyasa wananchi, kuteka watu akiwamo Mo wa Simba na polisi walivyokwenda hospitali kuwateka watu waliokuwa wakitibiwa na kwenda kuwaua.

Ameendelea kudai kuwa katika video hiyo inamuonyesha Zitto akielezea namna Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alivyoshindwa kuwadhibiti askari wake.

Shahidi huyo amesema Zitto anamfahamu tangu akiwa Chadema ni mfuasi wake na hadi leo akiwa ACT Wazalendo.

Amedai binafsi alimuamini kutokana na taarifa hiyo akaona polisi hawana thamani kama wameshindwa kulinda raia na mali zao.

Katika kesi hiyo, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kutenda Oktoba 28, 2018 katika mkutano uliofanyika ofisi za makao makuu ya ACT- Wazalendo.