VIDEO: Shahidi aeleza alivyomshuhudia Mbowe akihamasisha maandamano

Wednesday May 15 2019

Mchomelea ,vyuma ,alivyoshuhudia, maandamano , Chadema ,

Freeman Mbowe 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, ameeleza jinsi alivyomshuhudia mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akihamasisha maandamano kuelekea kwa mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni.

Shahidi huyo E 6976 koplo Rahim Ramadhani, askari polisi kituo cha Oysterbay ameeleza hayo leo Jumatano Mei 15, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akitoa ushahidi wa kesi inayowakabili viongozi hao wa Chadema.

Akiongozwa na wakili wa Serikali,  Wankyo Saimon, shahidi huyo ameeleza kuwa, Februari 16, 2018 aliingia kazini saa 12 asubuhi na kupangiwa kufanya doria wilaya ya Kinondoni akiwa na wenzake sita.

 

Amesema siku hiyo jioni wakiwa Mwenge (barabara ya Bagamoyo) wakiwa wameegesha gari walipigiwa simu ya upepo na OCD Dotto na kupewa maelekezo kwa askari Mohammed Selengi kuelekea viwanja vya Buibui Mwananyamala.

 

Advertisement

Amedai kuwa katika viwanja hivyo  kulikuwa na mkutano wa Chadema unaoendelea ambako kuna viongozi waliokuwa wanatoa maneno ya uvunjifu wa amani wakiwa jukwaani.

 

Shahidi huyo ameeleza kuwa katika mkutano huo walitakiwa kwenda kuongeza nguvu na walipofika walipanga askari katika mkutano ule.

 

Amesema kuwa alimshuhudia Mbowe akichukua kipaza sauti kutoka kwa aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni, kutamka kuwasindikiza viongozi waliokuwa eneo lile kwenda kwa mkurugenzi huyo kuchukua barua zao.

 

Amebainisha kuwa katika mkutano huo watu walikuwa wengi  na alikuwa ameshatoa rai na kurudisha kipaza sauti kisha kushuka kwenye jukwaa ambapo wananchi waliokuwa kwenye uwanja ule walikuwa na hasira zilizosababishwa na viongozi akiwemo Mbowe.

 

Ameeleza kuwa wananchi walitaharuki na kuwa na hasira na walitoa kauli za uvunjifu wa amani kwa kusema, “hatuogopi, hatutishiki, tutaandamana hadi kieleweke.”

 

Wakiwa katika viwanja hivyo shahidi huyo ameeleza kuwa  Mselengi aliitwa kwa simu ya upepo akitakiwa kurejea Mkwajuni kwa kuwa maandamano yalikuwa yakiendelea.

Shahidi huyo amedai walipita barabara za pembezoni na walipofika Mkwajuni walimkuta mkuu wa operesheni wa mkoa.

 

Ameeleza walipofika waliamriwa kushuka kwenye magari wakati huo maandamano yakiwa yanaendelea huku waandamanaji wakisema hawaogopi mtu huku wakiwa wamebeba mawe, wengine kujifunika nyuso zao.

 

Amesema Afande Ngichi alitoa ilani akiwataka watawanyike  lakini waandamanaji hawakutaka kusitisha maandamano.

 

Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicenti Mashinji;  naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara); mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

 

Wengine ni mbunge wa Bunda,  Esther Bulaya;  mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na John Heche (Tarime Vijijini).

 

Mbowe na viongozi hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi, ikiwemo kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa na kufanya mkusanyiko usio halali.

 

Advertisement