Shahidi aeleza bosi wake alivyoongozana na gari lenye shehena ya dhahabu

Muktasari:

Koplo Meksela, shahidi wa nne katika kesi ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 319 yenye thamani ya Sh27. 8 bilioni ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza jinsi alivyolifungulia geti gari iliyokuwa imebeba shehena hiyo lilipokuwa likiingia na kutoka katika kituo kikuu cha polisi Mwanza, likiongozwa na bosi wake.

Mwanza. Koplo Meksela, shahidi wa nne katika kesi ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 319 yenye thamani ya Sh27. 8 bilioni ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza jinsi alivyolifungulia geti gari iliyokuwa imebeba shehena hiyo lilipokuwa likiingia na kutoka katika kituo kikuu cha polisi Mwanza, likiongozwa na bosi wake.

Shahidi huyo, akiongozwa na wakili wa Serikali,  Robert Kidando ameeleza hayo leo Jumatano Mei 22, 2019 akibainisha kuwa Januari 4, 2019 saa 3:00 usiku akiwa kwenye lindo  kituoni hapo aliamuliwa aruhusu magari mawili, moja la polisi na jingine dogo la binafsi.

“Nilisikia honi ya gari kutokea getini ilikuwa gari la polisi ndani yake alikuwamo Afande Okinda (mshatakiwa wa tano ambaye alikuwa operesheni ofisa) akiwa  anaendeshwa na afande Kasala. Afande Okinda alinieleza kwamba hata lile gari dogo ameongozana nalo niliache  liingie ndani," amesema shahidi huyo.

Amebainisha kuwa baada ya magari hayo kuingia kituoni hapo, waliteremka zaidi ya watu wanane lakini aliwatambua wanne,  askari watatu akiwemo Okinda na Kasala na mtu mwingine mwenye asili ya Kihindi aliyekuwa amevaa kanzu nyeupe ambaye hamjui jina.

Amedai baada ya kuingia ndani walielekea moja kwa moja hadi ofisi ya Okinda na kukaa kwa takribani saa moja na kisha kuondoka wakitumia magari hayo.

Wakili wa upande wa utetezi, Steven Makwega amemuuliza shahidi huyo kama yeye alikuwa mlinzi wa jengo hilo kwa nini hakuyakagua magari hayo yalipoingia ndani.

Hata hivyo shahidi huyo akijibu swali hilo amedai kwamba asingeweza kumkagua Okinda kwa kuwa ni bosi wake.