Shahidi aeleza kilichozungumzwa na Zitto polisi

Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe akijadiliana jambo na wakili wake Steven Mwakibolwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kesi kuanza.

Muktasari:

Salum Masoud, shahidi wa nne katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa taarifa aliyotolewa na mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) katika vyombo mbalimbali vya habari ni yake

Dar es Salaam. Salum Masoud, shahidi wa nne katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa taarifa aliyotolewa na mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) katika vyombo mbalimbali vya habari ni yake.

Shahidi huyo ambaye ni mkuu wa upelelezi Mkoa wa kipolisi Kinondoni ameeleza hayo leo Ijumaa Mei 17, 2019 akidai kuwa  Zitto alipohojiwa alikiri kufanya mkutano na waandishi wa habari unaohusu “Serikali kuvuruga zao la korosho, imeshindwa kulinda ustawi na usalama wa raia.”

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi,  shahidi huyo amedai Oktoba 31, 2018  akiwa kituo cha Polisi cha Oysterbay mkuu wa upelelezi Mkoa wa kipolisi Kinondoni (RCO), Albert Katundu aliongozana na Zitto katika ofisi ya upelelezi kwa ajili ya mahojiano.

Amesema mbunge huyo ambaye ni kiongozi wa ACT-Wazalendo alifika polisi baada ya kupata barua kutoka kwa RCO kwamba anahitajika kwa mahojiano kutokana na maneno ya uchochezi dhidi ya Serikali aliyoyatoa.

Amebainisha kuwa wakati Zitto akihojiwa, yeye alikuwa pembeni akisikiliza na mbunge huyo alikiri kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Shahidi huyo alieleza baada ya mahojiano alimuomba Zitto ampatie  taarifa ya maandishi iliyokuwa imeandaliwa kwa vyombo vya habari siku ya mkutano wake, alikubaliwa na mbunge huyo akisema atamtuma kijana wake kuileta.

Amesema kijana huyo alileta taarifa hiyo na kumkabidhi Zitto ambaye aliitazama na kukiri kuwa ni yake.

Amesema baada ya kuipitia alimtaka Zitto kusaini fomu ya makabidhiano na alikubali huku akimuomba, Gabriel Katengo asaini kama shahidi wake.

Shahidi huyo amebainisha kuwa taarifa hiyo yenye kurasa sita imesainiwa na Zitto na aliikabidhi kwa RCO na kuiomba mahakama kupokea nyaraka hizo kama kielelezo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 18 na Juni 19, 2019 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi akidaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.