Shahidi akwamisha kesi ya Zitto
Muktasari:
- Kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe imeshindwa kuendelea katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na shahidi kutofika mahakamani
Dar es Salaam. Kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe imeshindwa kuendelea katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na shahidi kutofika mahakamani.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga amedai leo Jumanne Januari 29, 2019 mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shahidi kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini amepata matatizo ya kifamilia na kushindwa kufika.
“Kwa jinsi upande wa mashtaka tulivyokuwa tumejipanga tulitaka tuanze na ushahidi leo na shahidi tuliyekuwa tumemuandaa amepata matatizo ya kifamilia tunaomba kuahirishwa kwa muda,” amesema Katuga.
Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai mshtakiwa alikuwa amejiandaa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini pia ana majukumu mengine kuomba tarehe za mwishoni.
Hakimu Shahidi baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, 2019 kwaajili ya kuanza kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka.
Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.
Alifikishwa katika mahakama hiyo na kushtakiwa kwa mashtaka matatu ya uchochezi.