Shahidi augua mahakamani, akwamisha kesi ya ‘Mpemba wa Magufuli’

Wednesday July 24 2019

 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kusikiliza ushahidi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli’ kutokana na shahidi kuugua.

Yusuf na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni.

Wakili wa Serikali, Elia Athanas amedai leo Jumatano Julai 24, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na shahidi yupo tayari.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa tunaye shahidi mmoja Daniel Gumbo hivyo tuko tayari kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji,” amedai  Athanas.

Shahidi huyo alipotakiwa kuanza kutoa ushahidi alidai mahakamani hapo kuwa  kichwa kinamuuma hivyo hataweza kuendelea kutoa ushahidi.

Wakili wa utetezi Juma Nassoro aliiomba Mahakama kumuonya shahidi huyo ili tarehe itakayopangwa aweze kufika kwaajili ya kesi hiyo kuendelea.

Advertisement

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14 na 15, 2019 itakapoendelea na ushahidi na kuutaka upande wa mashtaka kuleta shahidi zaidi ya mmoja kwa kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu tangu mwaka 2016.

Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Yusuph(35), washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 53/2016.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh 392.8 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Advertisement