Shangazi mbaroni akidaiwa kumuunguza mtoto wa kaka yake, kisa kukojoa kitandani

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Emmanuel Nley,

Muktasari:

  • Anadaiwa alitumia banio la moto kutekeleza ukatili huo. Baba mtu aliamua kutolripoti tukio hilo lakini msamaria mwema akatoa taarifa polisi

Polisi mkoani Tabora inamshikilia mkazi wa Malolo, Mwanjaa Salum (47) kwa tuhuma za kumuunguza mtoto wa kaka yake (miaka mitatu) kwa madai ya kukojoa kitandani.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Emmanuel Nley,  akizungumza leo Mei 16, 2019, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Mei 13, 2019 baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia mwema.

Amedai kuwa mtuhumiwa alimuunguza mtoto huyo sehemu mbalimbali za mwili wake lakini hasa mapajani.

Amebainisha, “baba wa mtoto aitwaye Yusufu Hassan, baada ya dada yake kumfanyia ukatili mwanawe huyo, pengine kwa lengo la kumlinda dada yake aliamua kumpeleka kwa mama yake mzazi eneo la Ng'ambo, Manispaa ya Tabora.”

Amesema mtoto huyo hivi sasa anatibiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete na hali yake inaendelea vizuri.

Amewataka wananchi kutoa taarifa mapema za matukio ya unyanyasaji kwa lengo la kukomesha vitendo hivyo.

Diwani wa Kata ya Malolo, Cornel Ng'wandu amesema hana taarifa za kukamatwa kwa mkazi wake huyo na anafuatilia kufahamu zaidi kuhusu tukio hilo.

Akizungumzia matukio ya ukatili na unyanyasaji, diwani huyo amesema hakuna kwenye eneo lake.