Shibuda atoa neno kwa vyama vya siasa Tanzania

Muktasari:

  • Mwenyekiti  wa baraza la vyama vya siasa nchini Tanzania,  John Shibuda amevitaka vyama vya siasa kuendelea kuwa kinga na  ngao dhidi ya mambo yanayoweza kusambaratisha Taifa

Moshi. Mwenyekiti  wa baraza la vyama vya siasa nchini Tanzania,  John Shibuda amevitaka vyama vya siasa kuendelea kuwa kinga na  ngao dhidi ya mambo yanayoweza kusambaratisha Taifa.

Shibuda ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 20, 2019 katika uzinduzi wa safari mpya ya treni ya mizigo ya Tanga-Kilimanjaro uliofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

"Wanasiasa tuliopo hapa tuendelee kuwa kinga na ngao dhidi ya vita ovu inayoweza kusambaratisha Taifa. Vita ya mwanasiasa ni chama na chama, adui mkubwa wa  mwanasiasa ni maradhi, ujinga na umaskini, "amesema Shibuda.

Akizungumza kwa niaba ya makatibu wa vyama vya siasa katibu wa chama cha ADC,  Doyo Hassan amesema vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kuishauri Serikali na wana imani na kazi zinazofanyika.

Amemuomba Rais John Maguful kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na kuzungumza nao kama alivyofanya kwa viongozi wa dini na wengine.

“Nakuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kamwambie Rais viongozi wa vyama vya siasa wakiwa wenyewe wanakubali kazi inafanyika lakini ametutenga katika kumsaidia mawazo kumshauri kama alivyofanya kwa viongozi wa dini,” amesema.