Shirika la Tehama la Afrika Kusini kuwekeza Tanzania

Muktasari:

  • Kampuni ya utoaji wa huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kutoka nchini Afrika Kusini, imeonyesha dhamira ya kuwekeza nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi na taasisi mbalimbali zinazohitaji kwenda sanjari na mabadiliko ya kidunia katika huduma za mawasiliano

Dar es Salaam. Shirika linalojihusisha na biashara katika huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) la Afrika Kusini, limeonyesha dhamira ya kuwekeza Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi na taasisi mbalimbali zinazohitaji kwenda sanjari na mabadiliko ya kidunia katika huduma za mawasiliano.

Shirika hilo la CHPC lilianzishwa mwaka 2007 katika mji wa Pretoria, Afrika Kusini na kwa sasa inafanya biashara ya kutoa huduma na bidhaa katika nchi zaidi ya kumi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Baadhi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na shirika hilo lenye ubia na Serikali ya Afrika ya Kusini ni pamoja na ufungaji wa miundombinu ya mawasiliano katika ofisi, ufungaji wa mfumo mpya katika  kompyuta, uzalishaji wa programu za kompyuta, uunganishaji wa huduma za internet.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Agosti 6,2019 Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania katika siku ya pili ya maonyesho ya bidhaa kwa wiki ya viwanda kwa nchi 16 za SADC, Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Happy Sithole amesema kwa sasa wameanza kufanya utafiti wa awali kwa lengo la kujiridhisha na mazingira ya uwekezaji,

“Tunahitaji kufahamu pia masuala ya sera za kibiashara, mahitaji ya soko na utayari wa kampuni za Tehama zitakazohitaji kushirikiana, kutokana na matokeo nitakayoyapata, itanishawishi miaka kadhaa tu ijayo kurejea kuwekeza Tanzania, ”amesema Dk Sithole aliyeweka banda la huduma zake

“Tunamiliki IP yetu (Intellectual property) Katika nchi tulizofika SADC, tumekuwa tunawezesha kwanza wataalamu kutumia mifumo ya huduma zetu, baada ya hapo tunafanya biashara, hatuhofii jambo lolote tunapotoa mafunzo kuhusu uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma za teknolojia tunayotoa,” amesema.

Tayari wafanyabiashara wageni 172 kati ya 1,576 wa nchi 16 za Jumuiya hiyo wamejitokeza kuanzia jana Jumatatu kuanza kutangaza bidhaa zao kwa lengo la kukuza mtandao wa masoko ya Nchi za SADC kupitia bidhaa zake.

Kwa mujibu wa wizara ya viwanda, tayari washiriki 3,001 wameshajisajili kushiriki mikutano ya SADC, wakitokea nchi za SADC ikiwamo Tanzania.