Shirika la Viwango Tanzania kuanza usajili wa majengo ya uzalishaji wa chakula

Sunday June 30 2019

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Kuanzia kesho Shirika la Viwango Tanzania (TBS), litaanza kutoa usajili wa majengo ya uzalishaji wa chakula na vipodozi, kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa za chakula zinazozalisha nchini na zinatoka nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja  baada ya Bunge la Tanzania kupitisha muswada wa Sheria (The finance bill 2019) ambao baada ya kusainiwa utaleta mabadiliko ya Sheria ya Viwango namba 2 ya mwaka 2009 (sura130), ambapo TBS imeongezewa majukumu ya kudhibiti ubora wa usalama wa chakula na vipodozi.

Awali, majukumu hayo yalikuwa yakitekelezwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Taarifa iliyotolewa leo  Jumapili Juni 30, 2019 kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Athuman Ngenya  imeeleza kuwa  cheti  cha usajili wa majengo kwa wazalishaji walioko nchini, kitaendelea kutambuliwa na TBS hadi muda wake wa miaka mitano utakapokwisha. Baada ya muda huo usajili utatolewa na TBS.

Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, TBS itaendelea pia na utaratibu wa kutoa usajili wa majengo ka waombaji wapya kwa kutumia mfumo ulioainishwa na kuzingatia matakwa ya usalama na ubora  wa chakula na vipodozi.

“Usajili mpya utaendelea kadri vyeti vya usajili wa majengo vilivyopo vitakapoisha muda wake. Tofauti na awali. Upimaji wa  sampuli utafanyikia mara moja kwa bidhaa zilizokidhi matakwa yote mawili ya usalama,  ubora wa chakula na vipodozi kwa mujibu wa viwango husika kwenye ukaguzi wa mwanzo.

Advertisement

“Hatua hii inalenga kupunguza gharama na muda wa upimaji, ni vema mzalishaji kuhakikisha anajiandaa katika kudhibiti usalama, ubora wa chakula na vipodozi,” imeeleza taarifa hiyo.

kuhusu  bidhaa za chakula na vipodozi kutoka nje ya nchi, TBS itaendelea kutambua usajili wake uliopitia TFDA na udhibiti wa bidhaa hizo zinapoingia nchini, utafanyika kwa mfumo wa udhibiti ubora uliyoanishwa ili kukidhi matakwa yake.

Advertisement