Shule iliyokuwa ya tisa kutoka mwisho imefungiwa kuchukua wanafunzi

Mkuu wa Wilaya ya Chemba , Simon Odunga

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga ameelezea mambo ambayo yamesababisha Shule ya Sekondari ya Mondo kushika nafasi ya tisa toka mwisho katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita.

Dodoma. Shule ya Sekondari ya Mondo ambayo imeshika nafasi ya tisa katika shule 10 za mwisho kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha Sita, imefungiwa kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu baada ya kubainika ina upungufu katika miundombinu yake.

Akizungumza na Mwananchi  jana Alhamisi Julai 11, 2019 kwa simu, Mkuu wa Wilaya ya Chemba iliko shule hiyo, Simon Odunga amesema wilaya hiyo ina changamoto ya mwamko wa elimu, watu wengi wanapenda sana elimu ya dini kuliko ya darasani.

“Changamoto tunayokutana nayo ni kuleta ule mwamko wa elimu kwa wananchi wa Chemba. Matokeo mazuri yanategemea jitihada za wazazi pia, hata kama Serikali inafanya jitihada kubwa ya kuboresha mazingira ya elimu,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Amesema ili matokeo yaweze kuwa mazuri pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali, lazima wazazi waone kuwa elimu ni kipaumbele chao.

Amesema kwa upande wa Serikali walikuwa na changamoto za kimiundombinu kwamba, shule hiyo ilifungiwa kupokea wanafunzi wa kidato cha tano, mwaka jana.

“Moja ya vigezo vilivyofanya wafungiwe ilikuwa ni miundombinu, hakukuwa na usalama katika mabweni kwa mfano kukosekana kwa uzio, maabara na maktaba,” amesema.

Hata hivyo, Odunga amesema tayari wanaendelea na ujenzi wa miundombinu kwa kupeleka maji, kujenga uzio na yale yote walioambiwa na wakaguzi wa ubora elimu kuwa ni kikwazo, wametekeleza kwa asilimia 80.

Amesema hilo linawafanya kuamini kuwa mwaka huu wanapopanga wanafunzi watawapanga kwasababu tayari vikwazo wamehaviondoa.

Amesema kuwa pia wanaupungufu wawalimu wa sayansi na hisabati ambayo yalikuwa hayafundishwi kabisa katika shule hiyo na hali hiyo imetokana na upungufu wa walimu katika wilaya hiyo.

“Shule nyingine ambazo tungetegemea kuchukua walimu na kuwapeleka katika shule hizo bado pia upungufu upo kwa hiyo inaweza  kuwa ni kikwazo kwasababu baadhi ya masomo hayajafundishwa kabisa,”amesema.

Odunga amesema  kuwa watoto hao wanaweza wakawa walifanya mitihani kwanamna ya ubabaishaji tu.

“Jitihada zimefanyika za kupeleka walimu. Tutahakikisha mambo yanayotuhusu tunayatekeleza,”amesema.