Shule yashangaa kushika mkia, askari mbaroni akidaiwa kuhujumu

Mmoja ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Masjadi Qubah iliyopo jijini Dar es Salaam akiingia ofisini shuleni hapo jana. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Katika matokeo hayo, Masjadi Qubah ndio imeshika mkia kitaifa huku Kwizu ikiwa ya tatu kutoka mkiani.

Dar/ Mikoani. Shule za sekondari Kwizu na Masjadi Qubah zilizo miongoni mwa 10 zilizofanya vibaya kitaifa mtihani wa kidato cha nne 2018, zimetaja sababu ya kutofaulisha vizuri, huku mkuu wa shule ya Kwizu, Peter Mngulwi akisema matokeo yamewashangaza kwa kuwa wanafunzi wao walijiandaa vizuri.

Mbali ya shule hizo, zingine zilizofanya vibaya kitaifa ni Pwani Mchangani (Kaskazini Unguja), Ukutini (Kusini Pemba), Kwediboma (Tanga), Rwemondo (Kagera), Namatula (Lindi), Kijini (Kaskazini Unguja), Komkalakala (Tanga) na Seuta (Tanga).

Wakati Masjadi Qubah na Mkwizu zikitoa ufafanuzi wa matokeo mabaya waliyoyapata, askari PC Hamisi wa Kituo cha Polisi Malinyi anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kujihusisha na udanganyifu wa mitihani hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa aliliambia Mwananchi jana kuwa, askari huyo alishiriki kufanya udanganyifu huo wakati akisimamia mtihani katika Sekondari ya Tumaini Lutheran iliyopo wilayani humo.

Tuhuma za askari kujihusisha na udanganyifu zilitajwa pia juzi na katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde katika mkutano wake na wanahabari wakati akitangaza matokeo hayo.

Dk Msonde alisema walibaini udanganyifu uliohusisha utoboaji wa tundu katika ukuta ambapo mitihani hiyo ilikuwa ikipitishwa kwenda kwa walimu kupitia kwa wanafunzi wa kidato cha pili ili wakaifanye na kisha ilirejeshwa katika chumba cha mtihani na askari.

Katika matokeo hayo, Masjadi Qubah ndio imeshika mkia kitaifa huku Kwizu ikiwa ya tatu kutoka mkiani.

Akizungumzia matokeo hayo jana, mwalimu mkuu wa Sekondari ya Kwiuzu, Mngulwi alisema yamewachanganywa na hawakuyatarajia.

“Matokeo yametuchanganya hatujui nini kimetokea. Wanafunzi walijiandaa vizuri sana na tulitarajia matokeo mazuri, nashindwa kuelewa shida ni nini. Niko kwenye state of shock (hali ya mshtuko),” alisema Mngulwi.

Kwa mujibu wa Mngulwi, wanafunzi wote 70 walifanya vizuri katika mitihani ya majaribio ukiwamo ule wa Mock na mtihani wa Taifa wa kidato cha pili, lakini matokeo hayo yamekuja kinyume na matarajio yao.

Mwalimu huyo alisema atafanya uchunguzi wa kina kujua kilichosabbaisha matokeo mabaya hadi shule yake isiingie katika 10 bora kitaifa, na baadaye atawaeleza Watanzania.

Msimamizi mkuu wa maboresho ya shule ya Masjadi Qubah, Omary Said alisema sababu ya kufanya vibaya ni uongozi mbovu na wanafunzi waliofanya mtihani huo kuchukuliwa kutoka shule nyingine.

“Nakumbuka miaka ya 2000 shule hii iliwahi kufutiwa matokeo kwa sababu ya ufaulu uliotia shaka. Tangu shule ilipofutiwa matokeo ilianza kuyumba kidogo kitaaluma na hata kiutawala na mwaka 2016 mmiliki alitaka kuibadilisha kuifanya chuo cha ualimu,” alisema Said.

Alisema wakati akiwa katika harakati za kuibadilisha, baadhi ya wanafunzi walihamishiwa shule zingine za jirani kwa kupewa uhamisho.

“Ilipofika mwezi wa saba 2017 mmiliki akakwama kufanya usajili wa shule kuwa chuo, hivyo bodi ya shule ikaamua kuvunja mkataba na mmiliki wa shule.”

Alisema, “Kuanzia hapo kukawa na mkanganyiko wa utaratibu wa kuendesha shule, hivyo bodi ikafanya maamuzi ya kurejesha mfumo wa awali yaani wa kuendelea kuwa shule na sio chuo.”

Said alisema waliamua kutafuta wanafunzi wa kuanza nao kwani tayari wengi walikuwa wamehamishiwa shule nyingine, ikiwamo kuwarejesha wale ambao walisoma hapo waliohamishiwa shule nyingine.

“Pamoja na yote hayo tupo kwenye tathmini ya maboresho ya shule, tunataka kuirejesha upya iwe ni shule bora, ndiyo maana unaona tupo hapa tunafanya ukarabati wa majengo.”

St Marks, St Mathews

Kufuatia Necta kuzuia matokeo ya watahiniwa 381 wa shule za St Marks na St Mathews zilizopo Temeke, Dar es Salaam na Mkuranga mkoani Pwani, jana wazazi walikuwa wakipishana katika shule hizo kujua hatima ya watoto wao.

Mmoja wa wazazi aliyezungumza na Mwananchi, Hilda Yosef alisema: “Nimekuja kuuliza (matokeo) yatatoka lini, lakini majibu niliyopata sio rafiki kabisa.”

Wakati mkuu wa shule ya St Marks, Leticia Joseph akisema wanasubiri kauli ya Necta, mkuu wa shule msaidizi wa St Mathew, Nalaila Joseph alisema pia wanafuatilia katika baraza hilo.

Katibu mtendaji wa Necta, Dk Msonde alisema hawezi kuzungumza hatima ya shule hizo akihofia kuwa ataharibu uchunguzi unaoendelea.

Serikali

Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha aliliambia Mwananchi jana kuwa mfumo wa mtihani una udhibiti mkali na ni rahisi udanganyifu wowote unaofanyika kubainika kwa urahisi.

“Wale watumishi ambao watabainika kuwa walihusika katika wizi wa mitihani hii watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufukuzwa kazi ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia kama hiyo,” alisema Ole Nasha.

Imeandikwa na Jackline Masinde, Aurea Simtowe, Kalunde Jamal na Tausi Ally (Dar), Daniel Mjema (Moshi)