Sijui nimfanyeje mke wangu jamani maana hanipi muda wa kupumzika

Pole kwa kazi Anti. Nimeoa huu mwaka wa pili, najaribu kumrudisha mke wangu awe kwenye hali ya kawaida nimeshindwa labda unaweza kunipa ushauri nifanye nini. Mke wangu anataka nikutane naye kimwili zaidi ya mara tatu kwa siku.

Nimejitahidi lakini kadri siku zinavyokwenda ninashindwa, ikitokea nimeshindwa ananuna siku nzima.

Nifanyeje?

Inawezekana ana hamu na wewe kutokana na mapenzi yake juu yako.

Lakini pia inawezekana ana tatizo la kisaikolojia lililotokana na tukio fulani alilopitia huko nyuma.

Kwa sababu hatujampima na kujua anasumbuliwa na nini, nakushauri kwanza mpeleke kwa mtaalamu wa saikolojia wapo wengi unaweza kuchukua namba kwenye magazeti ikiwamo hili, azungumze anye anaweza kubaini chanzo cha kuhitaji tendo hilo mara nyingi.

Iwapo mtaalamu wa saikolojia hatobaini tatizo, mpeleke kwa mtaalamu wa masuala ya homoni inawezekana ana tatizo huko.

Naamini kwa wataalamu hawa utapata ufumbuzi wa tatizo hilo, usisahau kumtanguliza Mungu pia kwa maombi na dua.

Hawa tulionao wanatushinda

Mume wangu anataka tuzae watoto watano, hivi sasa tunao watatu na hali ya kipato siyo nzuri tumelazimika kuwahamishia shule za umma kutoka binafsi, kila nikimwambia tupumzike kwanza hataki anatishia kuniacha.

Kama unaona wazazi wake wana uelewa washirikishe ukiwapa sababu za kimaisha lakini za kiafya pia.

Pia washirikishe viongozi wa dini ukijenga hoja za kimaisha ambazo mnakutana nazo lakini umuhimu wa kupaishanisha watoto kwa ajili ya mustakabali wao.

Kuna kitu nataka ujifunze pia. Epuka kumwambia akiwa na hasira, hana fedha, zungumza naye akiwa na furaha na ametulia.

Kwa hali hii uvumilivu utanishinda

Anti nimevumilia vya kutosha naona uvumilivu utanishinda, mume wangu ananipiga hadi navimba mwili mzima. Kwetu niliambiwa nisitoe siri za ndani nje, hivyo navumilia lakini naona atakuja kuniumiza.

Nimelileta kwako unishauri nifanye nini?

Vipo vitu vya kuvumilia lakini siyo kipigo, hata waliokuambia usitoe siri za ndani nje hawakumaanisha kuficha kipigo, walimaanisha masuala ya unyumba na magomvi ya kawaida.

Sasa upatapo ujumbe huu nenda dawati la jinsia ambalo lipo karibu.

Hii siyo kwako pekee bali kwa wanawake wote hakuna kanuni ala sheria ya ndoa inayosisitiza mtu kuvumilia kipigo.

Kumbuka wapo watu wengi wamefariki kwa kupigwa.