Siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya kitaifanya kufanyika kesho Tanga

Muktasari:

  • Serikali imeendelea kusimamia utoaji tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo, na kufanikiwa kuongeza idadi ya waathirika wa dawa za kulevya katika vituo vya tiba

Dar es Salaam. Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, kesho Jumatano Juni 26, 2019 inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya kwa lengo la kuikumbusha jamii juu ya tatizo kubwa lilipo hivi sasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Juni 25,2019 na Kitengo cha mawasiliano Serikalini ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari inasema maadhimisho hayo yatafanyika Kitaifa mkoani Tanga yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Waathirika wa Dawa za Kulevya Wana Haki ya Kupata Huduma za Afya.’

kuzingatia Kauli mbiu hii inakumbusha kuwa mapambano dhidi ya Tatizo la Dawa za Kulevya yanahitaji mikakati mtambuka na jumuishi ikiwemo suala la tiba kwa waathirika. Ni muhimu kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya kupata tiba stahiki na zilizothibitishwa kisayansi (evidence based practices) ili kuweza kupunguza madhara ya dawa hizo kwa waraibu na jamii inayowazunguka. Baada ya tiba hizo, huduma endelevu za Stadi za Kazi pamoja na Ushauri Nasaha kuzingatiwa ili kuwasaidia waathirika wasirudi kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, mkakati huu unaenda sambamba na mkakati wa utoaji wa elimu kwa vijana ili wasiingie kwenye matumizi ya Dawa za Kulevya pamoja na Udhibiti wa wafanyabiashara wa Dawa hizo.

 

Maadhimisho haya ni fursa kwa umma wa Watanzania kwa vile  Tatizo la Dawa za Kulevya linaathiri nchi yetu katika nyanja za kiafya, kijamii, kiuchumi pamoja na kutishia ulinzi na usalama wa nchi yetu.  Katika maadhimisho haya Watanzania  wataweza kupata elimu na kukumbushwa kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana athari kubwa kwa mtumiaji, kwa jamii na kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Taarifa hiyo inasema tatizo la dawa za kulevya husababisha madhara kiafya yanayochochea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi, virusi vya homa ya ini aina ya B na C, kifua kikuu, magonjwa ya akili, na usugu wa tiba ya kifua kikuu na Ukimwi.

“Baadhi ya dawa za kulevya husababisha matatizo ya uzazi kama upungufu wa nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo ya akili na kuenea kwa kansa mbalimbali kama ya koo, mapafu na mara nyingine husababisha vifo vya ghafla vitokanavyo na dozi kuwa kubwa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, inaelezwa kuwa Serikali inaendelea kusimamia utoaji wa tiba kwa waathirika wa dawa hizo kwa lengo la kupunguza madhara yanayotokana na matumizi yake.

Inasema mwaka 2015, waathirika wa dawa za kulevya waliokuwa wakitibiwa kwenye vituo vya tiba ni wagonjwa 2,400 mwaka 2015 na kufikia mwaka jana kulikuwa na wagonjwa 7,000.

“Hali hii imesaidia kupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa waraibu wa dawa za kulevya wanaojidunga kutoka asilimia 35 mwaka 2015 hadi asilimia 18.5, mwaka 2018.

Pia, Serikali inamtaka kila mwananchi kwa nafasi yake katika jamii kushirikiana na vyombo vya dola kuwabaini wote wanaouza na kutumia pia.