Silinde, Zitto walivyochuana na mawaziri wa Fedha ukuaji wa uchumi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akimuonyesha Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe (kushoto) barua ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoonyesha kwamba halikuhusika na taarifa zilizovuja kuhusu ripoti ya ukuaji wa uchumi wa nchi, bungeni jijini Dodoma jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alisema hata kama makisio ya IMF hayatumiki na makadirio ya Serikali yakatumika, bado ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia sita ni chini ya uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Dodoma. Wabunge Zitto Kabwe na David Silinde, wamesema licha ya Serikali kutenga kiasi kikubwa cha bajeti kwenye miradi ya ujenzi na uchukuzi, sekta hizo hazichangii katika ukuaji wa uchumi. Hoja za wabunge hao zimeibukia katika majadiliano ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyowasilishwa bungeni mjini hapa juzi na Waziri Issack Kamwelwe.

Wa kwanza kuchangia alikuwa Silinde ambaye ni mbunge wa Momba (Chadema), aliyenukuu kile alichodai kuwa ni ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), akisema inaonyesha uchumi wa Tanzania utakua kwa wastani wa asilimia nne 2019, licha ya fedha nyingi kuwekezwa katika sekta ya ujenzi.

“Ripoti ya IMF inaonyesha uchumi wetu utakua kwa asilimia 4.4 mwaka huu, kwa nini hali hii inatokea wakati ukuaji ulikuwa wastani wa asilimia saba kwa muongo mmoja uliopita na fedha nyingi tunazielekeza kwenye ujenzi,” alihoji Silinde.

Hoja hiyo ilimlazimu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kusimama na kutoa taarifa akisema, “hii niliyoshika ni ripoti ya IMF. Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) inakadiria uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6.8 na Benki ya Dunia inakadiria uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.6 mwaka 2019. Hiyo taarifa unayoitumia ni ile iliyovuja,” alisema Dk Mpango.

Aliposimama, Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Waziri pango na Naibu wake, Dk Ashatu Kijaji walisimama na kutoa taarifa kwa nyakati tofauti.

Zitto alisema kwa miaka mitatu iliyopita Serikali imewekeza Sh18.7 trilioni kwenye sekta ya ujenzi ambayo duniani kote inaongoza kuchangia kukuza uchumi, lakini hali ni tofauti hapa nchini.

Alisema fedha hizo zimewekezwa kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ndege na miradi mingine mikubwa ambako hazijawekezwa kimkakati ili kulinufaisha Taifa.

“Tunajenga sana miundombinu lakini mchango wake bado ni mdogo, sababu wakandarasi wa wanaopewa miradi hii wanatoka nje, hivyo fedha za ununuzi wa malighafi wanapeleka nje pia,” alisema.

Alitoa mfano Kenya waliojenga SGR kwa mkopo lakini mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi ni asilimia 1.5, akashangaa Tanzania iliyowekeza kiasi kikubwa kasi inapungua.

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alisema hata kama makisio ya IMF hayatumiki na makadirio ya Serikali yakatumika, bado ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia sita ni chini ya uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Alisema Serikali inakusanya fedha kutoka kwa wauza nyanya kisha mapato hayo yanakwenda nje kununua malighafi za ujenzi wa miradi, jambo linalopunguza mzunguko wa uchumi na kasi ya ukuaji wake

Dk Mpango

Alipopewa nafasi ya kutoa taarifa, Waziri Mpango alitoa takwimu za ukuaji wa pato la Taifa 2013 akisema lilikua asilimia 6.8, mwaka 2014 asilimia 6.7 na 2015 asilimia 6.2.

Alisema 2016 uchumi ulikua kwa asilimia 6.9, mwaka 2017 asilimia 6.8 na 2018 kwa asilimia 6.9.

Hata hivyo, ingawa miradi inayotekelezwa inaonekana, Zitto alipokea taarifa ya waziri na kusema kuwa muundo wa utekelezaji wa vipaumbele unapaswa kuangaliwa ili kuhakikisha fedha zinazotumika zichochee uchumi.

“Naomba Serikali iseme uwekezaji wa Sh18.7 trilioni kwenye ujenzi uliofanywa kwa miaka mitatu iliyopita umezalisha ajira ngapi za kudumu, viwanda vingapi na umechochea vipi sekta ya kilimo,” alisema.

Ingawa alikubaliana na takwimu za Dk Mpango, Zitto alisema IMF hawajakanusha makisio waliyoyatoa, bali ripoti iliyovuja. “Hakuna mtu asiyetaka nchi yake isiendelee. Utekelezaji wa sera za kiuchumi kwa miaka minne iliyopita ni mbovu ndiyo maana fedha nyingi zinatolewa lakini uchumi haukui.”

Maelezo hayo ya Zitto yalimsimamisha Dk Kijaji aliyesema faida za uwekezaji katika sekta ya ujenzi siyo za muda mfupi na kwenye ukuaji wa uchumi wa asilimia 6.9 wa mwaka jana, sekta ya ujenzi ilichangia asilimia 12.9.

Zitto hakupokea taarifa hiyo, lakini alisema kuna tofauti kubwa kati ya kasi ya ukuaji wa uchumi na uchumi wenyewe. “Sekta ya ujenzi ni ya pili kwa kasi ya ukuaji siyo ya pili kuchangia, lakini upili wake hauonekani kwenye ukuaji wa uchumi na hiyo ndiyo hoja yangu.”