Simulizi ya ng’ombe 20 wanaosakwa na Lugola

Muktasari:

Waziri huyo ameagiza vigogo wawili wa vyombo vya usalama mkonia Kagera kuripoti ofisini kwake Dodoma ikiwa ni baada ya kumzungusha bila kumpatia nyaraka alizozihitaji kuhusiana na suala hilo

Biharamulo. Simulizi ya mkazi wa kijiji cha Nyambale wilayani Biharamulo, Bilatwa Mabuga aliyedai ng’ombe wake 20 kukamatwa na polisi tangu 2017 wakati akiwapeleka kwenye mnada wa Lusahunga wilayani humo, imewaweka mtegoni vigogo wawili wa polisi na magereza.

Kutokana na simulizi ya mama huyo katika mkutano wa hadhara mjini hapa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewabana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi na Mkuu wa Magereza mkoani humo, Raymond Mwampashe alioagiza wafike ofisini kwake Dodoma wakiwa na vielelezo ili wajieleze.

Bilatwa alisema juzi kuwa ng’ombe hao baada ya kukamatwa alitakiwa kuwasilisha vielelezo kuthibitisha umiliki wake.

Alisema hata baada ya kuwasilisha vielelezo na nyaraka za kuthibitisha umiliki wa mifugo hiyo aliyosema ni mali ya Luhembeja Mkama, polisi wameendelea kuishikilia tangu Septemba 22, 2017.

“Baada ya kutoa vielelezo, polisi wa kituo cha Lusahunga walinidai rushwa ya Sh1 milioni waliyonielekeza kuituma kwa njia ya mtandao na niliposhindwa kutekeleza agizo hilo ndipo nilipoambiwa mifugo yangu imehamishiwa magereza (Biharamulo) ili ikatunzwe. Nimefuatilia bila mafanikio hadi leo,” alidai Bilatwa.

Kufuatia malalamiko hayo Lugola aliagiza Malimi na Mwampashe wafike Dodoma Januari 16 wakiwa na vielelezo vya kukamatwa kwa mifugo hiyo.

Akizungumza baada ya kusubiri kupatiwa vielelezo hivyo kwa zaidi ya saa mbili bila mafanikio, alitaja vielelezo anavyohitaji kuwa ni vile vinavyoonyesha na kueleza jinsi mifugo hiyo ilivyokamatwa, iliyofia njiani wakati ikisafirishwa kwenda kuhifadhiwa katika mashamba ya Gereza la Biharamulo na taarifa ya uchunguzi wa daktari wa mifugo kuelezea sababu za vifo hivyo.

Waziri huyo pia aliwataka kumpatia hati ya makabidhiano ya mifugo hiyo kati ya polisi na wenzao wa magereza.

Awali, baada ya kupokea malalamiko hayo na kukosa majibu mwafaka kutoka kwa viongozi hao wa vyombo hivyo vya ulinzi na usalama waliokuwepo kwenye mkutano huo, Lugola aliusitisha saa 11:45 jioni na kwenda eneo la Gereza la Biharamulo kupata nyaraka na kujiridhisha iwapo mifugo hiyo ipo.

Alipofika alisubiri kupatiwa nyaraka bila mafanikio hadi ilipofika saa 2:20 usiku alipoamua kuondoka na kutoa maagizo hayo.