Sintofahamu ya kifo cha Hamza Bin Laden na anguko la Al Qaeda

Ikiwa imepita miaka minane tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda, Osama bi Laden kundi hilo limeendelea kuwepo na likibeba ama vitisho au kuhusika katika matukio mbalimbali ya kigaidi.

Likiwa chini ya Osama kundi hilo linakumbukwa zaidi kwa kutekeleza mashambulizi ya Septemba 11 (2001), yaliyoacha vilio visivyosahaulika katika taifa kubwa na lenye nguvu duniani la Marekani ambapo maelfu ya watu walipoteza maisha na maelfu wengine kujeruhiwa.

Kushambuliwa balozi za Marekani katika muda unaokaribiana nchini Kenya na Tanzania, Agosti 7, 1998, ni miongoni mwa matukio ambayo kwa ukanda wa Afrika Mashariki yanatosha kuwa sababu ya kulikumbuka kundi hilo chini ya Osama.

Mara baada ya Osama kuuawa na vikosi vya Marekani huko Pakistan Mei 2, 2011, Al Qaeda iliendeleza operesheni zake za kigaidi chini ya Ayman al-Zawahiri ambaye hata hivyo sasa inaelezwa kuwa ni mgonjwa na uwezo wake katika kuliongoza kundi hilo umedorora.

Tegemeo kubwa kwa maendeleo ya Al Qaeda liliwekwa kwa mmoja wa watoto wa Osama ambaye tangu enzi za uhai wa baba yake alionekana kuwa karibu naye zaidi na hata kuaminiwa na wapiganaji wa kundi hilo na hivyo iliaminika huenda baada ya Al-Zawahiri, Hamza bin Laden angekamata usukani.

Hata hivyo mambo yamekwenda tofauti baada ya vikosi vya Marekani kuripoti kuwa Hamza ameuawa katika moja ya operesheni za taifa hilo lenye nguvu kubwa za kijeshi.

Na ingawa taarifa hizo hazijathibitishwa na Al Qaeda wenyewe lakini ukimya wa Hamza na kundi hilo unatosha kutoa ishara zote kwamba Hamza ni kweli ameuawa.

Hamza bin Laden

Taarifa zilizotolewa na mmoja wa maofisa wa ujasusi wa Marekani ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa jina, zilisema nchi yake inaamini Hamza ameuawa katika moja ya operesheni zilizoendeshwa na majeshi yao.

Hata hivyo, ofisa huyo alikataa kutoa maelezo zaidi kuhusiana na jambo hilo ikiwamo kuweka wazi ni lini na mahali gani alikokutwa na kuuawa kijana huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30.

Rais Donald Trump, Jumatatu iliyopita alikataa kuzungumza chochote kuhusu taarifa za kuuawa kwa Hamza zilizorushwa mara ya kwanza na kituo cha Televisheni cha NBC. “Siwezi kuzungumza chochote kuhusiana na hilo.”

Hamza ni mmoja wa watoto 23 wa Osama bin Laden na ambaye inaelezwa alikuwa karibu sana na baba yake wakati wa uhai wake huku akiwekwa katika orodha ya wanaosakwa kwa kuwa sehemu ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Inaaminika Hamza alikuwa na baba yake Afghanistan kabla ya mashambulizi ya Al Qaeda ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani na kusababisha hasara kubwa mbali na vifo na majeruhi maelfu kwa maelfu.

Inadaiwa baadaye aliondoka na baba yake kwenda mafichoni Pakistan baada ya Marekani kuanzisha msako dhidi ya Osama na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuusambaratisha mtandao wa viongozi wa juu wa kundi hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, Marekani imekuwa na uhusika kwa kiasi kikubwa katika operesheni iliyofanikisha kuuawa kwa Hamza takribani miaka miwili iliyopita.

Hata hivyo, Februari mwaka huu, Marekani ilitangaza kutoa zawadi nono ya dola milioni moja (zaidi ya Sh2.2 bilioni), kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa kiongozi huyo wa juu wa Al Qaeda popote alipo, hali ambayo inaweza kuleta sintofahamu kuhusu kifo cha Hamza.

Mwaka 2015 inaaminika alitambulishwa rasmi na Ayman al-Zawahiri kwa wapiganaji wa kundi hilo akiaminika atakuwa kiungo muhimu cha kurudisha nguvu ya Al Qaeda ambayo kwa miaka ya karibuni imeonekana kufifia huku kundi lingine lenye mrengo kama huo la ISIS likionekana kuchukua nafasi yake.

Kwa nini anahofiwa?

Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail Online, inaaminika Hamza ana nguvu ya ushawishi ambayo ingeweza kutumika kuwarudisha pamoja na kuwaunganisha wapiganaji wa Al Qaeda ambao wametawanyika sehemu mbalimbali ingawa bado ni tishio na hatari kwa usalama wa maeneo mbalimbali.

Amewahi kuhamasisha matukio ya kigaidi kwa nchi za Magharibi huku binafsi akiapa kulipa kisasi kwa Marekani kutokana na mauaji ya baba yake.

Mwaka 2017 Marekani ilimuorodhesha Hamza katika orodha ya magaidi duniani. Mbali na hilo, inaelezwa kuwa Hamza alihamasisha mashambulizi dhidi ya Wamarekani nje ya nchi yao huku akiyataka makundi ya kikabila nchini Saudi Arabia kuungana na tawi la Al Qaeda lililoko Yemen.

Machi mwaka huu, Saudi Arabia ilitangaza kumvua Hamza uraia wa nchi hiyo ikielezwa kuwa uamuzi huo unatokana na agizo la mfalme wa nchi hiyo lililotolewa Novemba 2018.

Watoto 23 wa Osama wanaofahamika

Inadaiwa hadi anafariki mwaka 2011, Osama bin Laden alifanikiwa kupata watoto 23 kutokana na wake zake watano aliowahi kuwaoa enzi za uhai wake.

Watoto kutoka tumbo la mke wake wa kwanza, Najwa (59) ni Abdullah bin Laden (43), Abdul Rahman bin Laden (41), Sa’ad bin Laden (30), huyu aliuawa kutokana na mashambuzlizi ya angani yaliyofanywa na Marekani nchini Pakistan mwaka 2009.

Wengine ni Omar bin Laden (38) ambaye mwaka 2006 alimuoa mwanamke mzaliwa wa Uingereza Jane Felix-Browne. Baadaye Jane alisema Omar anataka kuwa balozi wa amani kati ya Waislamu na mataifa ya Magharibi.

Kwa mke wake huyo pia alizaliwa Mohammed bin Laden (36), Osman bin Laden (36), Fatima bint Laden (32), Laden bin Laden (30), Iman bin Laden (29), Rukhaiya bint Laden (22), Nour bint Laden (20).

Kwa Siham Sabar, walizaliwa Miriam bint Laden (29), Sumaiya bint Laden (27), Khalid bin Laden, ambaye aliuawa sambamba na baba yake akiwa ni umri wa miaka 23 mwaka 2011.

Kwa Amal al-Sadah (36) walizaliwa watoto watano; Safiyah bint Laden (18), Aasiah bint Laden (16), Ibrahim bin Laden (15), Zainab bint Laden (13) na Hussein bin Laden (11). Na kwa Kwa Khadijah Sharif (71); walipatikana Ali bin Laden (33), Amer bin Laden (29) na Aisha bint Laden (27).