Siri ya Hamisa Mobetto kupata dili hii hapa

Muktasari:

Umewahi kujiuliza sababu za mwanamitindo, Hamisa Mobetto kupata dili za ubalozi wa kampuni mbalimbali nchini Tanzania ikilinganishwa na mastaa wengine wanawake


Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza sababu za mwanamitindo, Hamisa Mobetto kupata dili za ubalozi wa kampuni mbalimbali nchini Tanzania ikilinganishwa na mastaa wengine wanawake.

Meneja mkuu wa kampuni ya vifaa vya ujenzi ya Dar Ceramica, Celestine Gunda amesema urembo si kigezo pekee kinachomfanya Hamisa kupata dili hizo.

Akimtangaza Hamisa kuwa balozi wa kampuni hiyo Celestine amesema walivutiwa na namna anavyojiweka na kujitofautisha na mastaa wengine.

Amesema kingine ni jinsi mrembo huyo anavyoweza kujielezea mbele za watu na kuonekana kuwa na ushawishi wa kuwafanya watu wamsikilize.

Pia, umahiri wake katika kutangaza na kuzielezea bidhaa ni sifa nyingine inayoshawishi kampuni, taasisi na mashirika kumpa ubalozi.

“Hamisa ni msichana mrembo lakini kampuni yetu haikuangalia urembo wake pekee bali sifa nyingine za ziada ambazo zimetushawishi kufanya naye kazi na kwa muda mchache tuliokuwa naye tumeona mafanikio makubwa,” amesema Gunda.

Licha ya kuwa ujenzi na masuala ya urembo ni vitu viwili tofauti Hamisa ameahidi kutekeleza jukumu lake hilo jipya kwa ufanisi wa hali ya juu.

 

“Nashukuru kazi za watu nazifanya vizuri ndio sababu wanaendelea kuniamini na dili kama hivi zinakuja, ninachoahidi ni kufanya vile inavyotakiwa na kuanzia sasa kila Jumamosi nitakuwa kwenye maduka na showrooms zetu kuuza bidhaa,” amesema Hamisa.

 

Kuhusu anavyoweza kutekeleza majukumu yote aliyonayo,  Hamisa anasema siri kubwa ni kupangilia muda wake kwa kuzingatia kazi anazotakiwa kufanya.

 

Amesema anaandaa ratiba ya kila siku na ndiyo maana licha ya kuwa na majukumu mengi anaweza kuhakikisha hayaingiliani.

 

Pamoja na kazi zote alizonazo mrembo huyu anaeleza kuwa muda anaopumzika nyumbani huwa anajitahidi kuutumia kuwa karibu na watoto wake.

 

“Mara nyingi huwa nasafiri au kuwa na majukumu mengi lakini inapotokea nipo nyumbani najitahidi niwe karibu na watoto wangu napenda sana kutumia muda  ninaoupata kuwa na wanangu,” amesisitiza.

 

Ukiachana na ubalozi wa bidhaa, kampuni na taasisi mbalimbali binafsi na za umma, Hamisa pia ni mwanamuziki na mjasiriamali kupitia duka lake la Mobettostyles.