Siri ya kupata mafanikio sekta ya anga nchini yatajwa

Wanafunzi wa kozi ya uhudumu wa ndani ya Ndege wa Chuo Cha Usafiri wa Anga na Utalii cha Swissport Tanzania wakipanda Ndege jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda  kufanya mafunzo kwa vitendo.Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Wanafunzi wanaochukua mafunzo hayo wapo tisa na wawili kati yao ni wanaume, walisafiri na shirika la ndege la Precion Air kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar kisha Kilimanjaro na kurudi tena Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Maendeleo yanayofanywa katika sekta ya anga nchini yanapaswa kwenda sambamba na uzalishaji wa wataalamu ili kuifanya sekta hiyo kuendelea kukua zaidi.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na mkurugenzi wa kampuni ya Swissport Tanzania, Mrisho Yassin baada ya wanafunzi wa kwanza wanaosoma kozi ya uhudumu ndani ya ndege (Cabin Crew) katika chuo cha usafiri wa anga na utalii kinachomilikiwa na kampuni hiyo kuanza mafunzo kwa vitendo

“Sekta ya usafiri wa anga ina uhitaji mkubwa wa wataalamu na sisi hatuwezi kukidhi mahitaji yote lakini tunapunguza katika maeneo kadhaa hususan huduma kwa wateja na udhibiti wa mizigo,” alisema Yassin ambaye msingi mkubwa wa biashara ya kampuni anayoiongoza ni udhibiti wa mizigo katika viwanja vya ndege.

Alisema hakuna shirika lolote la ndege ambalo wameingia nalo makubaliano ya kuchukua wahitimu katika chuo hicho, lakini ana imani kuwa wanafunzi wote watapata ajira pindi watakapohitimu kwa kuwa soko la ajira katika sekta hiyo ni kubwa na elimu inayotolewa ina ithibati ya kimataifa hivyo mhitimu ataweza kufanya kazi na shirika lolote.

“Tunaaminiwa na watu wengi na tumekuwa tukifanya kozi kwa wadau wa usafiri wa anga wanafahamu kuhusu ubora wa kozi zetu hivyo hawatakuwa na wasiwasi na wanafunzi tunaowatoa, wanafunzi wengine ambao wanasoma kozi zinazoendana na shughuli zetu kama za kudhibiti mizigo tunapokuwa na nafasi tunawachukua wenyewe,” alisema Yassin.

Wanafunzi wanaochukua mafunzo hayo wapo tisa na wawili kati yao ni wanaume, walisafiri na shirika la ndege la Precion Air kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar kisha Kilimanjaro na kurudi tena Dar es Salaam.

Wakiwa ndani ya ndege walishirikiana na wahudumu wa shirika hilo kuwahudumia abiria ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo.