VIDEO: Sita wafariki dunia 361 wathibitika kuugua kipindupindu

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, wakati akitoa taarifa kuhusu hali ya ugonjwa wa ebola, kipindupindu na dengue nchini. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Serikali imesema jumla ya wagonjwa sita wamefariki dunia na wengine 361 wamethibitika kuugua kipindupindu tangu kutokea kwa ugonjwa huo Aprili jijini Tanga na Dar es Salaam, Mei mwaka huu.

Dar es Salaam. Serikali imesema mpaka sasa watu sita wamefariki dunia na wengine 361 wameugua kipindupindu mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu Leo Juni 17, 2019, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema hali iliyopo sasa inaridhisha kwa sababu wagonjwa wanaendelea kupungua.

“Wiki mbili nyuma kimeibuka kipindupindu katika jiji la Dar es Salaam, lakini kwa sasa hali inaanza kuwa nzuri wagonjwa wanapungua na ukifika kwenye kambi za Temeke, Amana na Mwananyamala utamkuta mmoja au wawili, Takwimu kwa nchi nzima watu sita wamefariki huku 361 wakiugua ugonjwa huu,” amesema Dk Ndugulile.

Aidha, alipoulizwa kuhusu hali ya homa ya dengue, amesema takwimu zinaendelea kupungua huku akisema Serikali itatoa majibu ya takwimu hizo mwishoni mwa mwezi huu.

"Ukusanyaji takwimu bado unaendelea na Wizara tutazitoa baadaye mwezi huu," amesema.