Siyanga aeleza walivyofanikiwa kudhibiti dawa za kulevya Tanzania

Muktasari:

Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Rogers Siyanga aeleza namna walivyofanikiwa kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya Tanzania.

Dar es Salaam. Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Siyanga amesema usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya nchini Tanzania umepungua kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na mamlaka hiyo.

Kamishna Siyanga ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 11, 2019 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu DCEA kuandaa kongamano la wasanii litakalofanyika Jumatano lenye lengo la kutoa elimu kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.

“Kwa sasa wasafirishaji wamekuwa wakitumia njia ya Msumbiji  inayopitisha dawa kutoka Pakistan na Iran, kabla ya kuingia hapa nchini. Sasa hivi hata wasafirishaji wakubwa wanabeba  wastani wa kilo moja mpaka tano,” amesema Siyanga.

Siyanga amesema hali hiyo imechangiwa zaidi baada ya kudhibitiwa kwa njia ya Kaskazini iliyokuwa ikitumiwa kupitisha dawa hizo kuelekea Urusi na njia ya Balkan iliyokuwa ikipitia nchi za Iran-Uturuki kisha kuingia mataifa mengine ya Ulaya .

Kwa mujibu wa Siyanga, kiwango  cha tani  9,000 kilikamatwa kwenye eneo la bahari ukilinganisha na nchi kavu ambapo tani 1,000 zilipatikana katika kipindi cha mwaka 2018.

“Tumeongeza nguvu kwenye mpaka wa Kusini ili kuzuia uingizwaji dawa za kulevya, tunakusudia kuandaa vipeperushi vitakavyoelezea madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na vitasambazwa kwa jamii,” amesema Siyanga