Sokoine ni waziri mkuu aliyekuwa na mashati matatu, suruali tatu na viatu pea mbili

Saturday April 13 2019

 

Ilikuwa saa 10.00 alasiri ya Aprili 12, 1984 wakati Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ilipokatisha ghafla matangazo yake ya kawaida kisha kupigwa wimbo wa Taifa.

Kukatishwa kwa matangazo hayo ilikuwa ni kupisha taarifa ya huzuni iliyotolewa na Rais Mwalimu Nyerere akisema:

“Ndugu wananchi, leo saa saba mchana, ndugu na kijana wetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Edward Moringe Sokoine alipokuwa akisafiri kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake ilipata ajali. Amefariki dunia.”

Jana ilikuwa miaka 35 tangu Sokoine afariki dunia alipokuwa akitokea bungeni mjini Dodoma akirejea Dar es Salaam.

Maadhimisho ya kumbukumbu yake yalifanyika Monduli mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salam, Kardinali Polycarp Pengo.

Pengo katika maadhimisho hayo alizungumza namna Sokoine alivyokuwa kiongozi mwadilifu na mwenye maisha ya kawaida licha ya kuwa na nafasi kubwa katika uongozi wa nchi.

Advertisement

“Hayati Sokoine enzi za uhai wake aliacha viatu pea mbili tu, hapo ndio muone ni jinsi gani alikuwa hana ubinafsi alikuwa akipigania maslahi ya nchi yake, bila kujali maisha aliyokuwa akiishi, na mfano huu unatakiwa kuigwa na viongozi wetu wa sasa kwani kwa kufanya hivyo tutalifikisha Taifa letu mbali,” alisema Pengo.

Kauli ya pengo inakumbusha yaliyosemwa na Mwalimu Nyerere wakati wa mazishi ya Sokoine huko Monduli.

“Edward Sokoine hakuwa na yoyote. Ukiacha ng’ombe alioachiwa urithi na wazazi wake alikuwa na mashati matatu, suruali tatu na viatu pea mbili,” alisema Mwalimu Nyerere wakati wa mazishi ya Sokoine.

Sokoine aliishi maisha ya kawaida tofauti na wadhifa wake huo wa juu kabisa ukiwa ni wa tatu baada ya Rais, wakati huo akiwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa Rais alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi. Kwa sasa Mwinyi ni Rais mstaafu wa awamu ya pili.

Akizungumza kwenye kumbukumbu ya miaka 35 ya Sokoine, Askofu Pengo aliwataka viongozi na wananchi wa kuiga mfano wa

Sokoine kwa kutokuwa wabinafsi huku wakitanguliza masilahi ya nchi mbele.

Anasema Sokoine alipiga vita ubinafsi na watu kujilimbikizia mali katika kuhakikisha wananchi wote wanapata haki sawa, hivyo hayo yote yanapaswa kuendelezwa katika nchi yetu ili tuendelee kuishi kwa amani na upendo.

Pengo anasema Sokoine ni kati ya viongozi walioendeleza amani ya Taifa na alikuwa mchangiaji katika uendelezaji wa amani wa Taifa, hivyo ataendelea kukumbukwa kwa juhudi zake za kutetea masilahi ya nchi na kupiga vita ubinafsi.

Mongela amuelezea Sokoine

Kutoka Morogoro mwandishi wetu, Hamida Shariff anaripoti kuwa mwanasiasa mkongwe, Getrude Mongela amesema hawezi kuyasahau maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa na Edward Sokoine saa chache kabla ya kupata ajali na kufariki dunia.

Mongela aliyasema hayo jana mjini hapa wakati wa kongamano la kumbukizi ya hayati Sokoine lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) ambapo aliyataja baadhi ya maagizo na maelekezo kuwa ni pamoja na namna ya kujenga uchumi mpya wa nchi ulioathirika na vita ya Kagera dhidi ya Idd Amini.

Anasema kuwa Sokoine akiwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya kwanza siku moja kabla ya kifo chake kabla ya kuahirisha Bunge alizungumza na mawaziri na wakuu wa mikoa na kutoa maelekezo mbalimbali na baadaye aliandaa chakula cha usiku na kuwaalika viongozi hao.

Mongela anasema kuwa katika hafla hiyo Sokoine alihakikisha chakula kinaandaliwa vizuri ambapo alikwenda mwenyewe jikoni na kusimamia maandalizi ya chakula na baadaye alisimama mlangoni na kumkaribisha kila aliyemwalika katika hafla hiyo.

Mongela anasema baada ya hafla hiyo kumalizika Sokoine aliagana na viongozi hao lakini cha kushangaza asubuhi ya Aprili 12 aliwaita viongozi wachache akiwemo yeye (Mongela na Paul Kimiti) na kuwasisitiza tena yale aliyoagiza usiku na baadaye alianza safari ya Dar es Salaam.

Mongela alisema kuwa muda mfupi baada ya Sokoine kuanza safari naye alianza safari ya kuelekea Dar es Salaam na alipofika eneo la Dakawa Mvomero alikuta askari wengi wakiwa wanasimamisha magari huku kulia mwa barabara aliona gari lenye namba za Serikali likiwa limepinduka.

“Kitendo cha kuona gari la Serikali limepata ajali na mimi kama kiongozi wa Serikali nikateremka kwenye gari langu kwa lengo la kutaka kujua na ghafla askari mmoja ambaye nadhani hakujua kama mimi ni kiongozi aliniambia kwamba waziri mkuu Edward Sokoine amepata ajali na amekimbizwa hospitali ya Morogoro,” anasema Mongela.

Anasema kuwa hatua ya kwanza aliyoichukua baada ya kupata taarifa hizo aliondoka eneo hilo la ajali na kuwahi mjini Morogoro, hata hivyo wakati akiingia mjini Morogoro aliona ndege ya Serikali ikiwa inaruka angani huku wananchi wakilia na kuonesha masikitiko yao na alipouliza aliambiwa ndege hiyo ilikuwa imebeba mwili wa Edward Sokoine uliokuwa ukipelekwa Dar es Salaam.

“Baada ya kifo cha Sokoine nchi iliingia kwenye mshtuko na hata Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Rais wa awamu ya kwanza hakujua nini kitaendelea hasa katika suala zima la mabadiliko ya uongozi kwa kuwa tayari Mwalimu Nyerere alishatangaza kutoendelea na urais huku akionesha imani ya kumuachia nafasi hiyo hayati Edward Sokoine.

Akizungumzia namna Sokoine alivyoshiriki katika maendeleo ya kilimo, Mongela anasema kuwa katika uhai wake kama waziri mkuu alianzisha mashindano ya kilimo bora yaliyokuwa yakishindanishwa kwenye vijiji na kutoa zawadi kwa vijiji vilivyokuwa vikifanya vizuri.

Anasema Sokoine pia alipambana dhidi ya uhujumu uchumi, alihimiza kila mtu kufanya kazi kwa kujiamini na kufuata sheria na kusoma na ndio maana aliendelea kujiendeleza kimasomo hata baada ya kuwa Waziri mkuu.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anasema katika kumuenzi kwa vitendo Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia ikiwemo kujenga na kukarabati maabara, mabweni na karakana za kisayansi.

Kuhusu kufufua shule za kilimo ameahidi kusimamia na kuhakikisha ifikapo Januari 2020 shule hizo zinaanza kufundisha masomo ya kilimo ili kutoa fursa kwa wanafunzi wasiopata nafasi ya kufika chuo kikuu Sua kuweka kupata ujuzi wa kilimo

Mwanafunzi wa shule ya sekondari Mafiga manispaa ya Morogoro, Kishosha Musa akichangia mada aliiomba Serikali kuwafundisha vijana walioko kwenye shule za sekondari elimu ya uongozi ili waweze kuwa viongozi bora kama alivyokuwa Sokoine.

Awali, Makamu mkuu wa Sua, Profesa Raphael Chibunda alisema maadhimisho ya kumbukumbu ya Sokoine yamekuwa yakifanywa kila mwaka kwa kufanya midahalo na maonesho mbalimbali ya ubunifu wa kisayansi yanayoandaliwa na wanataaluma na wanafunzi wa chuo hicho.

Advertisement