Spika Ndugai asema Bajeti imelenga kuondoa utitiri wa kodi

Thursday June 13 2019

Mapendekezo, Bajeti  Serikali,  utitiri  kodi ,Mkemia Mkuu,Shirika  Viwango,

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mapendekezo ya Bajeti ya Serikali yaliyosomwa leo Alhamisi Juni 13, 2019 imerekebisha utitiri wa kodi uliokuwa ukilalamikiwa na wafanyabiashara pamoja na kuweka sawa vitengo korofi ambavyo ni  Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango (TBS), Mkemia Mkuu pamoja na Wizara ya Mifugo.

Amesema wabunge watakuwa na muda wa kujadili mapendekezo hayo kwa muda wa wiki nzima kuanzia Jumatatu ya Juni 17, 2019 kabla ya kupiga kura ya kila mmoja kwa jina lake ili kuipitisha.

Alizungumza hayo bungeni jijini Dodoma baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Ndugai amesema mapendekezo yaliyowasilishwa yameendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyokuwanayo wakati inaingia madarakani.

“Mapendekezo haya yamesheheni mambo mengi muhimu mazuri kwa nchi yetu, mambo mengi yameguswa katika kilimo, biashara, uvuvi, viwanda, uwekezaji, miundombinu, elimu, afya, maji hata mawigi yamekumbukwa safari hii,” amesema Ndugai.

Akizungumza kwa utani, Ndugai amesema “mapendekezo mengine yatawasilishwa wiki ijayo nafikiri kope, kucha, wanja yataletwa. Tunaipongeza sana Serikali, Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya mkiwa chini ya kiongozi wenu Rais wa Tanzania, John Magufuli.”

Advertisement

 

 

 


Advertisement