VIDEO: Spika Ndugai azungumzia idadi ya watu katika familia

Monday August 5 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema suala la idadi ya watu katika ngazi ya familia linatakiwa kuendana na kiwango cha uchumi katika familia husika ili watoto waweze kupata huduma za jamii kama vile elimu na afya.

Ndugai ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wabunge wa Afrika na Asia unaolenga kubadilishana uzoefu katika masuala ya idadi ya watu na maendeleo.

Amesema lazima nchi za Afrika zifikirie namna ya kugeuza idadi ya watu kama fursa ya kujiletea maendeleo lakini pia kudhibiti ongezeko la watu ili kila mtu katika ngazi ya familia hadi Taifa aweze kupata huduma muhimu.

“Lazima tuwe na idadi ya watu inayoendana na uchumi wetu; watu wangapi, hilo sasa linategemeana na kiwango cha uchumi katika ngazi ya familia, katika kiwango cha kaya na katika kiwango cha Taifa,” amesema Ndugai.

Spika Ndugai amesema Bunge la Tanzania litaendelea kuishauri Serikali kuhusu mambo mbalimbali ya idadi ya watu na maendeleo ili kuliwezesha Taifa hili kufikia dira yake maendeleo ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha wabunge wa Tanzania cha watu na maendeleo (TPAPD), Kassim Jamal amesema mkutano huo umekutanisha watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Asia kama vile Kenya, Uganda, Malawi, India, Japan, Thailand, Malaysia na Ufilipino.

Advertisement

“Kikao hiki kinalenga kubadilishana mawazo juu ya kukabiliana na ongezeko la watu na maendeleo. Ni fursa kwetu kujifunza wenzetu wanafanya nini ili sisi kama wabunge tuishauri serikali nini cha kufanya,” amesema Jamal ambaye pia ni mbunge wa Magomeni.

Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto amesema nchi yake inatambua umuhimu wa huduma ya afya kwa wote (UHC) ndiyo maana imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza malengo endelevu ya maendeleo (SDGs).

Advertisement