Sisi ni Taifa moja

Muktasari:

Hata kama kwa dakika 90, au kwa siku chache au kwa miezi michache ijayo, Taifa Stars imelifanya Taifa kuwa moja .

Dar es Salaam. Hata kama kwa dakika 90, au kwa siku chache au kwa miezi michache ijayo, Taifa Stars imelifanya Taifa kuwa moja.

Kazi iliyobaki ni kuendelea umoja huu. Hilo linajidhihirisha katika salamu za pongezi, zawadi, matamko kutoka kwa watu tofauti; wanasiasa, wafanyabiashara, taasisi kama Bunge na nyinginezo ambazo zimeweka kando tofauti zao na kushangilia kwa nguvu moja ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda ulioiwezesha Tanzania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kuzikosa kwa miaka 39.

Taifa Stars, timu ya soka ya Tanzania, sasa inaungana na mataifa mengine 23 kucheza fainali hizo zitakazofanyika Misri Juni 15 mpaka Julai 13 baada ya ushindi huo wa juzi Jumapili jioni.

“Jana (juzi) Watanzania wote wamefurahi na wameonyesha uzalendo wa kweli,” alisema Rais John Magufuli ambaye jana aliwaalika wachezaji wote Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kula nao chakula cha mchana.

“Pale kulikuwa hakuna mambo ya vyama, klabu, dini wala ukabila, bali utaifa na Utanzania kwanza ndiyo uliwekwa mbele.”

Rais alionyesha kutiwa moyo na namna wananchi walivyohamasika na kuweka kando tofauti zao na kuweka mbele uzalendo.

Alisema wakati wote wa mchezo Watanzania waliweka tofauti pembeni na kuvaa Utanzania jambo ambalo alisema lilimfurahisha.

Video iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais juzi, inamuonyesha Rais akitembea kwa furaha nyumbani kwake baada ya kuangalia mechi hiyo ya mwisho ya Kundi L , huku akieleza kuwa hicho ndicho alichokitaka.

“Haya ni matokeo mazuri naipongeza Taifa Stars na Watanzania kwa ujumla,” anasema Rais katika video hiyo.

“Timu yetu sasa iko vizuri. Nimefuatilia mchezo huu na sikutaka kwenda uwanjani. Taifa Stars oyeee! Tanzania oyeee.”

Alikuwa akipata chakula na wachezaji kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo Oktoba mwaka jana na kuipa Stars Sh50 milioni kusaidia maandalizi kabla ya kuivaa Lesotho.

Salamu nyingine zilitoka kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliyegusia jinsi mchezo huo ulivyounganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja.

“Naomba sana muelewane muende kama Watanzania na makandokando mengine muyaweke pembeni ili muweze kufika mbali kwa sababu tayari mmeshatwikwa zigo jingine,” alisema Samia.

Hali ya furaha ilitawala sehemu mbalimbali usiku wa kuamkia jana, hasa katika kumbi za burudani ambako nyimbo ambazo si kawaida kuchezwa maeneo hayo, ziliwekwa na watu kuimba na kushangilia.

Moja ya video zilizorushwa mitandaoni zinaonyesha pambio la “Hakuna Mungu Kama Wewe”, ambalo ni la dini ya Kikristo na ambalo limeimbwa na Kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama linachezwa kwenye ukumbi wa starehe na watu kuimba na kushangilia bila ya kujali tofauti zao za kidini.

Katika kumbi nyingine, Ma-DJ walicheza kibao cha “Mkono wa Bwana’ cha kundi la Zablon Singers na kusababisha kelele za shangwe.

Pia viongozi wa kisiasa, watu mashuhuri pamoja na mashirika ya umma na yale binafsi yametumia mitandao ya kijamii kuelezea furaha na kuipongeza Taifa Stars ambayo mara ya mwisho ilishiriki fainali hizo mwaka 1980 jijini Lagos Nigeria na ilifuzu kwa kuiondoa Zambia kwa bao la Peter Tino.

Akionyesha furaha yake, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliandika ujumbe wake kwenye akaunti ya Twitter.

“Taifa Stars leo mmenipa raha...ushindi mmoja ndio mwanzo wa ushindi mwingine. Kila la heri,” ameandika Rais Kikwete ambaye wakati wa utawala wake, alikuwa akilipa mishahara wa makocha wa timu za taifa, akiwemo Mbrazili Marcio Maximo wa Taifa Stars.

Kwa upande wa vyama, Chadema ilielezea ushindi huo kuwa ni mafanikio ya kujivunia kwa Watanzania wote.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, chama hicho kiliwataka Watanzania kutumia ushindi huo kudumisha mshikamano na umoja na kuhimiza maandalizi zaidi kwa ajili ya michezo ya fainali zitakazofanyika Misri.

Nayo CCM ilisema ushindi huo ni wa kimkakati. “Taifa Stars wametupatia namba ileile ya miradi mikubwa ya kimkakati, goli la 1: Stigler’s (Umeme); goli la 2 SGR (reli ya kisasa) na goli la 3, sekta ya anga (madege makubwa kama yote - ATCL),” ameandika Humphrey Polepole katika akaunti yake ya Twitter.

“Tunaona utekelezaji wa ilani ya CCM moja kwa moja. Heko Tanzania.”

Pia kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametumia akaunti yake ya Twitter kusema: “Nguvu ya mpira kuunganisha nchi ni ya aina yake. Kina @Samagoal10 kuwezesha Tanzania kufuzu ‘Mataifa Huru Afrika’ #AFCON nchi iliyokuwa imenuna, imejawa furaha. Hata Rais kuonyesha Umoja. Alivaa shati la zambarau, rangi ya Chama Cha @ACTwazalendo akitazama mechi Ikulu. #Tufurahi.”

Naye mfanyabiashara maarufu, Mohamed Dewji amesema: “Huu ni ushindi wetu sote... tumeandika historia mpya kwa nchi yetu, hongera Taifa Stars.”

Wakati mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam aliahidi kuwa baa zingeuza bia nusu bei, baadhi ya taasisi zinazotoa huduma, kama hospitali ziliweka punguzo la gharama ikiwa sehemu ya kusherekea matokeo hayo.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilitangaza punguzo kwa wagonjwa wa kulipia watakaofika hospitalini kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana.