Stephen Curry aiokoa Warriors na kipigo fainali za NBA

Muktasari:

Nyota huyo wa mpira wa kikapu aliiongoza timu yake kuzinduka katika robo ya mwisho ya mchezo wa pili wa fainali za Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA) na kuilaza Portland hivyo kuongoza kwa kushinda michezo 2-0.

 

San Francisco, Marekani/AFP. Stephen Curry leo alfajiri amefunga pointi 37 na kuiongoza Golden State Warriors kuepuka uwezekano wa kufungwa na Portland Trail Blazers baada ya kushinda kwa pointi 114-111 na hivyo kuongoza kwa michezo 2-0 katika mechi ya pili ya fainali za Ligi ya Mpira wa Kikapu za Kanda ya Magharibi.

Zikiwa zimesalia pointi nne mchezo kumalizika, Blazers ilikuwa ikiongoza kwa pointi 108-100 katika mechi hiyo kali iliyochezwa Oracle Arena.

Mapema katika mchezo huo, Trail Blazers ilichomoka mapema na kuongoza kwa tofauti ya pointi 17 mapema katika kipindi cha pili.

Warriors ilizinduka na kufunga pointi 39 katika robo ya tatu na kurudi mchezoni, lakini Portland, ikiongozwa na Damian Lillard, ikagangamaa.

Pointi tatu zilizofungwa na Meyers Leonard ziliifanya Portland iongoze kwa tofauti ya pointi nane mwishoni mwa robo ya nne, lakini baadaye Curry akashika hatamu.

Mipira mitatu ya adhabu aliyofunga Curry iliifanya Golden State iongoze kwa pointi 110-108, kabla ya three-pointer ya Seth--mdogo wake Curry-- kuiwezesha Portland kuongoza kwa pointi 111-110.

Lakini Kevon Looney akafunga kwa kudunk na kuifanya Golden State iongoze tena kwa pointi 112-111 zikiwa zimealia sekunde 52 kabla ya Draymond Green kufunga zikiwa zimesalia sekunde 12 mchezo kuisha na kuhitimisha ushindi huo.

"Tulijua watakuja kwa nia ya kushinda," alisema Curry.

"walitupa adhabu kubwa. Ile robo ya tatu ilikuwa ya aina yake. Kila mchezaji alionyesha jinsi alivyo."

Ilikuwa ni kiwango kingine kizuri cha mchezo kwa Curry, ambaye aliziba pengo la Kevin Durant ambaye ameumia na kuwezaz kufunga zaidi ya pointi 30 katika mechi mbili mfululizo za kwanza za fainali ya NBA.

Curry alimaliza mchezo huo akiwa amefunga pointi 37 kutokana na mipira 11 aliyofanikiwa kutumbukiza kiukapuni kati ya mipira 22 aliyorusha.

Katika mchezo huo, Klay Thompson aliiongezea Warriors pointi 24 wakati Green alimaliza akiwa amefunga pointi 16, Looney (14) na Jordan Bell (11).

Katika hatua nyingine, Portland imesema nyota wake, Durant, ambaye ameumia hataweza kucheza mchezo wa tatu na wanne wa fainali hizo kutokana na kuendelea kuuguiza matatizo ya misuli.