Suala la mgombea binafsi laibukia mjadala wa LHRC

Deus Kibamba

Muktasari:

  • Wadau mbalimbali wamesema ushiriki wa wananchi kwenye uongozi wa nchi ni mdogo kutokana na baadhi ya sheria kutotoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao.

Dar es Salaam. Suala la mgombea binafsi limeibuka tena kwenye mjadala wa hali ya ushiriki wa wananchi kwenye uongozi wa nchi katika kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania.

Mjadala huo umefanyika leo Jumanne Juni 25,2019 jijini Dar es Salaam na kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, vyombo vya habari, wanasheria na wanaharakati mbalimbali.

Akiwasilisha mada kwenye mjadala huo, mwanaharakati wa Katiba Mpya, Deus Kibamba amesema mpaka sasa hakuna mtu aliyechukua nafasi ya marehemu Christopher Mtikila katika kupigania suala la mgombea ni nafasi.

"Tangu Mtikila alipofariki dunia (Oktoba 4, 2015) suala la mgombea binafsi limetelekezwa, hakuna tena anayepigania mgombea binafsi wakati suala hili ni muhimu katika kushirikisha wananchi kwenye uongozi wa nchi yao,” amesema

Amesema Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinasema wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na watawala watapata mamlaka kutoka kwa wananchi.

Mbali na suala hilo, ameongeza kuwa kuna tatizo la kushambulia watu wenye maoni tofauti na kuwawekea vikwazo huku akitolea mfano mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Ayakuze ambaye alitoa utafiti ambao haukuzipendeza mamlaka za Serikali.