VIDEO: Sugu: Hata wapinzani humuunga mkono Rais Magufuli lakini haambiwi

Muktasari:

  • Viongozi wa upinzani humuunga mkono Rais John Magufuli ila huwa haambiwi na badala yake huambiwa yale ya kupinga pekee

Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu amesema yapo baadhi ya mambo ambayo viongozi wa upinzani humuunga mkono Rais John Magufuli ila huwa haambiwi na badala yake huambiwa yale ya kupinga pekee.

Amesema kutokana na hali hiyo yuko tayari kutumika katika kuondoa mafundofundo ya kisiasa yaliyopo katika mkoa wa Mbeya na hata kitaifa.

Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ruanda, Nzovwe jijini Mbeya leo Aprili 26, 2019.

Amesema suala la vitambulisho analiunga mkono kwa asilimia 100 huku akibainisha kuwa yapo mambo mengine wanayofanya hivyo.

“Mheshimiwa naibu Spika (Tulia Ackson) alizungumza na kusema yeye na wamachinga wenzake ila hata mimi ni mmachinga niliuza mitumba katika Soko la Mwanjelwa baada ya kumaliza kidato cha nne kabla ya kuingia katika muziki na nilikuwa naona shida zile,” amesema.

“Nilifurahi baada ya kusikia kuwa wamachinga wasibughudhiwe kwa sababu ndiyo mfumo wao wa ufanyaji biashara, hata Jengo la Machinga Complex limeshindwa kwa sababu ni ngumu kuwaweka wamachinga pamoja na badala yake wao ni watu wa kuzunguka tu.”

Amesema wafanyabiashara wa jiji la Mbeya pia wamekuwa wakilalamikia kodi na tozo nyingi huku Mamlaka ya Mapato wakishindwa kuweka utaratibu rafiki wa ukusanyaji kodi.

“Siyo kila mtu anaweza kuwa na utaalamu wa kodi, badala yake wawape elimu ili walipe kodi kwa hiari bila kushurutishwa.”

Changamoto ya maji

Akizungumzia changamoto ya maji katika jiji la Mbeya, Mbunge huyo alisema Sh70 bilioni zinahitajika ili kumaliza tatizo la maji huku chanzo chake ikiwa ni Mto Kiwila.

Amesema kwa mujibu wa wataalamu njia hiyo itakuwa ni tiba ya shida ya maji katika jiji la Mbeya na hata mkoa jirani wa Songwe.

“Hii inamaanisha katika maeneo yote ambayo bomba hili litapita watanufaika na maji na hata kupeleka katika mji wa Tunduma ambako nako kuna shida ya maji tutafikisha,” amesema Mbilinyi.