Sugu atoa neno, mwili wa Frank kukaa miezi saba na nusu mochwari

Marehemu Frank Kapange

Mbeya. Wakati mwili wa marehemu Frank Kapange (21) ukiendelea kuhifadhiwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa, Kanda ya Mbeya kwa siku 230, kutokana na mvutano wa kisheria baina ya familia na vyombo vya dola, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ameiomba Mahakama kuharakisha shauri hilo.

Frank alifariki dunia Juni 4 mwaka jana huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kuwa kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido jijini hapa alifariki kutokana kipigo akiwa mikononi mwa Polisi.

Kutokana na hali hiyo, waligoma kuchukua mwili kwa ajili ya maziko hadi jana mchana, ilielezwa kwamba mwili huo bado ulikuwa mochwari.

Akitoa maoni yake kuhusu shauri hilo, Mbilinyi ambaye ni maarufu ‘Sugu’ alisema anachopenda kuona kwa sasa ni mahakama kuharakisha jambo hilo ili likamilike mapema na haki ipatikane.

Alisema shauri hilo ambalo limechukua muda mrefu linagusa hisia za wengi.

Mbali ya Sugu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dk Stephen Mwakajumilo alitaka ubinadamu kutumika katika kumaliza suala hilo.

“Si utamaduni wetu Waafrika kuona mwili unakaa muda wote bila kuzikwa. Nawashauri tu wakauchukue mwili na kufanya maziko huku wakiendelea na suala la kesi mahakamani na Mahakama kama itaona kuna uhitaji kufanyika uchunguzi basi mwili utafukuliwa,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Teofilo Kisanji (Teku-Mbeya), Stella Seif alisema kutokana na mwenendo wa suala hilo, wanahitajika watu wenye busara ambao hawafungamani na upande wowote kama vile viongozi wa dini, wazee wa heshima na wa mila kuingilia kati ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo.

“Kwanza kuna tofauti mbili za familia, wapo ambao wanataka kuendelea na kesi mahakamani na wale ambao hawakubaliani nao, sasa hapo inakuja nani mwenye nguvu zaidi,” alisema. “Upande mmoja lazima utakuwa na nguvu kwa maana na kuheshimika kulingana na umri.

“Lakini hili kundi lisilokuwa na nguvu halitakuwa na uamuzi wowote ila wanaathirika kisaikolojia tu hivyo inahitaji busara zaidi kukaa na hii familia kuona namna ya kumaliza hili na kijana wao azikwe.

“Ninachokiona kwa sasa, kisaikolojia wawepo washauri na asiwepo anayetoka serikalini wala ndugu wa familia hiyo, bali wawe watu niliowataja.”

Msimamo wa familia

Kutokana na madai ya kifo cha Frank, ndugu walifungua shauri Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya kutoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi wa kifo hicho.

Mahakama hiyo ilitupilia mbali shauri hilo kwa maelezo kuwa halina mashiko na kuamuru mwili huo kuzikwa huku ikitaka ndugu kubeba gharama zote za mazishi.

Ndugu hawakuridhika na uamuzi huo wakaamua kukataa rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo ilitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kuwa mlalamikaji hakufuata taratibu wakati wa kufungua kesi hiyo.

Hata hivyo, Januari 3, wakili wa familia hiyo, Moris Mwamwenda aliliambia gazeti hili kwamba wanakwenda Mahakama ya rufani na sasa anachosubiri ni kuitwa na msajili wa mahakama hiyo ili kujulishwa kama shauri hilo limeshafanyiwa kazi ili awasilishe sababu za rufaa yake.