VIDEO: Sugu aachiwa kwa dhamana, atakiwa kuripoti polisi kesho

Muktasari:

  • Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu'  leo Alhamisi Februari 21, 2019 saa 1:00 jioni ameachiwa kwa dhamana muda mfupi baada ya kufikishwa kituo kikuu cha Polisi jijini Mbeya

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu'  leo Alhamisi Februari 21, 2019 saa 1:00 jioni ameachiwa kwa dhamana muda mfupi baada ya kufikishwa kituo kikuu cha Polisi jijini Mbeya.

Sugu alishikiliwa na polisi tangu saa 2:00 asubuhi baada ya kuripoti ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei  kwa ajili ya kuhojiwa.

Leo asubuhi Matei amesema Sugu alitakiwa kufika kituoni hapo kuhojiwa akidaiwa kutoa kauli za uchochezi, kukashifu mamlaka za Serikali alipokuwa akizungumzia ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo jijini Mbeya.

Ilipofika saa 9:00 alasiri alitolewa ofisi ya Matei na kupelekwa Shule ya Msingi Ikuti  alikodaiwa kutoa maneno hayo wakati akizungumza na wananchi alipokuwa akitoa misaada katika shule hiyo, kisha kurejeshwa kituoni.

Saa 1:00 jioni aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kesho asubuhi.

"Kesi iliyopo kwenye jalada wanasema ni ya uchunguzi  kwa hiyo tulipotoka makao makuu ya Polisi, tukaenda Ikuti ambako hatukukaa muda mrefu maana waliwahoji walimu kama sehemu ya uchunguzi. Niliporudishwa kituoni waliniweka mahabusu kama dakika 10 hivi na kuniachia kwa dhamana,” amesema Sugu.