MAWAIDHA YA IJUMAA: Suluhu ya mmomonyoko wa maadili katika jamii

Sheikh Muhammad Idd

Jamii kitaifa na kimataifa imekumbwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili. Maendeleo ya teknolojia hasa katika upande wa mawasiliano yamewezesha kupata ushahidi usio na shaka kwamba mmomonyoko wa maadili umefikia hatua mbaya isiyonyamazika wala kuvumilika.

Kwa Mtanzania yeyote, hahitaji kufahamishwa juu ya uwepo wa mmomonyoko wa maadili, labda anaweza kukwazwa na sababu pamoja na suluhisho.

Ni ukweli ulio wazi kwamba mmomonyoko wa maadili umeenea, haukuwabakisha wazee wala vijana, wanawake wala wanaume, viongozi wala wanaoongozwa.

Sote tunashuhudia mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu kwa kiwango ambacho wakubwa hawawahurumii kabisa wadogo na wadogo hawawaheshimu kabisa wakubwa.

Katika mazingira ya kazi, tunashuhudia baadhi ya wafanyakazi wakiwaibia waajiri wao na baadhi ya waajiri wanawadhulumu na kuwanyanyasa wafanyakazi wao.

Aidha, tunashuhudia wanaume wanavaa mavazi na mapambo ya wanawake na wanawake wanavaa mavazi ya wanaume. Na wakati mwingine wanawake badala ya kujisitiri wanavaa na wanatembea nusu uchi na pengine uchi kwa asilimia kubwa.

Vijana wa kiume wanathubutu kushiriki tendo la ndoa na mabinti wa watu kabla ya kuwaoa. Vijana wa kiume na kike wamefikia kutamani au hata kufanya uhusiano na mapenzi ya jinsia moja. Lakini mmomonyoko wa maadili umekwenda mbali zaidi kwa kiwango cha wazazi kutowajibika kulea watoto kimaadili bali kutekeleza mahitaji yao ya mavazi, chakula, malazi na masomo. Na watoto nao wamewatelekeza wazazi wao vijijini na wao wapo mijini ‘wakiponda’ raha.

Sababu ya maadili kumomonyoka

Miongoni mwa sababu kuu za mmomnyoko wa maadili ni jamii kujinyima na kunyimwa elimu ya dini, wazazi kutowajibika ipasavyo katika dhima ya kulea watoto wao na familia zao pamoja na watoto kutowajibika ipasavyo kuwaheshimu wazazi wao.

Pia, serikali kutokuwa na msimamo wa wazi nini inataka katika kulinda maadili na kupambana na athari za utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kuhusu jamii kunyimwa elimu ya dini, ni dini pekee ambayo ndiyo msingi mkubwa wa kulinda maadili. Quran Tukufu imemsifu Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) katika Sura ya 68 (Al-Qalam) Aya ya 4: “Na hakika wewe uko juu ya tabia tukufu” . Mwenyezi Mungu (Subhaanahuu Wataalaa) akamsifu tena Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) kupitia Quran Tukufu Sura ya 2 (Aali-Imraan) Aya ya 159: “Kwa sababu ya rehma itokayo kwa Mola wako (wewe Muhammad) umekuwa laini kwao, na lau wewe ungekuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangekukimbia…”

Aya hizo mbili zinaonyesha tabia njema alizokuwa nazo Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam). Kwa kuwa yeye Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) ndiye suluhisho la tabia njema, jamii ingeshika mafunzo yake ingefaulu.

Kuhusu wajibu wa wazazi kwa watoto wao, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Ni miongoni mwa haki za mtoto kwa mzazi wake kuifanya nzuri adabu yake na kulifanya zuri jina lake”

Na kuhusu wajibu wa watoto kwa wazazi wao, Mwenyezi Mungu amesema katika Sura ya 17 (Al-Israai) Aya ya 23: “Na Mola wako Mlezi ameamrisha msimuabudu yeyote ila Yeye Mwenyezi Mungu tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima”

Katika kusisitiza hilo, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema (nanukuu): “Radhi za Mwenyezi Mungu zinapatikana katika kuwaridhisha wazazi wawili na machukivu ya Mwenyezi Mungu yanapatikana katika kuwaudhi wazazi wawili” Mafunzo yote hayo yatapatikana kama jamii imeelimishwa juu ya dini. Hata suala hili la wazazi kutowajibika ipasavyo katika malezi ya watoto wao, nalo linachangiwa sana na jamii kukosa elimu ya dini.

Kwa ujumla, dini ni tiba kwani imani ya dini ndiyo anayotembea nayo mja muda wote. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Muogope Mwenyezi Mungu popote ulipo, na lifuatishie baya ambalo umelitenda kwa kufanya zuri na ishi na watu kwa tabia njema.’’

Serikali na maadili

Kuhusu Serikali kutokuwa na msimamo wa wazi juu ya nini inataka katika kulinda maadili, Serikali inawajibika kuwa makini katika tatizo hili la mmomonyoko wa maadili kwani athari yake inachangia pia kuua nguvu kazi ya nchi na kuleta uvunjifu wa amani.

Inapaswa kuwa makini kwani madhara ya mmomonyoko wa maadili ni makubwa na jamii imeyashuhudia kwa kiwango cha kutosha. Kwa mfano, kama wasanii waliovaa ‘nusu uchi’ wanaweza kupewa hadhi mbele ya viongozi wa Serikali, matarajio ni jamii kuiga na kuona si jambo baya kuvaa ‘nusu uchi’. Kama wasanii wa kiume waliovaa hereni, mikufu na kusuka nywele wanapewa heshima katika mikusanyiko ya Serikali, jamii itaiga uovu huo. Hivyo Serikali inabidi itoe msimamo wa wazi katika kulinda maadili mema ya Mtanzania na isijitenge katika wajibu huo kwani yenyewe ndio ‘baba mlezi’ haipaswi kukimbia ulezi.

Mwandishi wa makala haya ni mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. 0754 299 749, 0784 299 749.