TAMTHILIA YA SULTAN: Armstrong Dadi ndiye aliyemnakilisha Iskender Celebi

Wednesday January 9 2019

Iskander Celebi

Iskender Celebi katika tamthilia hii ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa ni Waziri wa Fedha katika himaya ya Ottoman na ni adui mkubwa wa Ibrahim Pasha.

Nafasi hii imechezwa na Hasan Kucukcetin, kijana wa miaka 37 na raia wa Kituruki. Mbali ya kuwa mwigizaji wa tamthilia na filamu, pia amekuwa akiendesha vipindi mbalimbali vya Televisheni.

Ameshawahi kucheza filamu mbalimbali ikiwemo Spring Never Comes (2013), Menekse ile Halil (2007 – 2008) na Sen Sag Ben Selamet ambayo ni ya mwaka 2016.

Armstrong Dadi

Amstrong Dadi ndiye aliyenakilisha sauti ya Iskender Celebi. Ni mmoja wa watu walionakilisha pia sauti katika katuni ya kirukuu, katuni iliyojizolea umaarufu miaka ya nyuma.

Pia amekuwa akiingiza sauti katika matangazo ya bidhaa mbalimbali.

Anasema ili uweze kufanya kazi ya kunakilisha ni lazima uwe msanii aidha wa kuigiza au mtangazaji.

Katika utangazaji anasema inakuwa rahisi kwani wengi wao hubadilisha sauti pale wanapotangaza vitu mbalimbali ikiwemo matangazo yanayoingia katikati ya vipindi. Hata hivyo anabainisha kuwa kuna tofauti kati ya kunakilisha sauti kwenye matangazo na tamthilia.

Kwenye tamthilia anasema unaweza kuwa na maneno 3,000 hadi 10,000 lakini kwenye tangazo la biashara utakuta una mistari mitatu.

“Hivyo katika tamthilia unaweza ukajikuta unatumia siku nzima kufanya kazi ya kunakilisha lakini kwenye tangazo ni muda mfupi tu utakuchukua huku pesa yake ikiwa ndefu, ”anasema Dadi.

Advertisement