TBS yazungumzia ubora wa bidhaa za Tanzania nchi za SADC

Muktasari:

  • Ni wazi kuwa ushindani katika soko hupimwa kwa ubora wa bidhaa. Bidhaa za Tanzania hazitaweza kuhimili ushindani bila ubora wa bidhaa.

Dar es Salaam. Ni wazi kuwa ushindani katika soko hupimwa kwa ubora wa bidhaa. Bidhaa za Tanzania hazitaweza kuhimili ushindani bila ubora wa bidhaa.

Umahiri wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) umesaidia kuchochea mazingira wezeshi ya bidhaa za Tanzania kupenyeza katika nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa mujibu wa TBS,  ina watalaamu wa kutosha na maabara tisa zenye vifaa vya kisasa zinazohusisha vipimo vya kemia, uhandisi wa umeme, uhandisi wa mitambo, ujenzi, chakula, ngozi, nguo na kondomu, pamba, ugezi (sayansi ya vipimo) na kituo cha teknoojia ya ufungaji.

Akizungumza na Mwananchi  leo Alhamisi Agosti 8, 2019 jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya mwisho ya maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi za SADC, ofisa uhusiano  wa shirika hilo, Neema Mtemvu amesema wanalazimika kujihakikishia ubora wa kila bidhaa inayotengenezwa Tanzania ili kusaidia ushindani na heshima ya bidhaa za Tanzania katika nchi za SADC.

“Kazi ya TBS ni pamoja na kumsaidia elimu ya kutosha mfanyabiashara anayeanza, tunampatia maelekezo baada ya kuona bidhaa yake haijakidhi vigezo vya kupata alama ya ubora na ndiyo siku ya uzalishaji  bidhaa yake tunakuwapo pale ili kumsaidia zaidi,” amesema Neema.

Kwa mujibu wa muundo wa kuoanisha viwango vya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi 16 za jumuiya hiyo (SADC- STAN), mashirika yote ya viwango katika nchi zote za SADC yanalazimika kuoanisha ubora wa bidhaa ili kuondoa vikwazo vya bidhaa ya nchi moja inapoingia nchi nyingine.

Pia, Muundo wa kuoanisha uwezo wa maabara na ugezi  inazitaka kila nchi mwanachama kuoanisha umahiri maabara zake kwa kutumia viashiria mbalimbali vya uwezo wa watalaamu wa vipimo, mazingira ya hali ya hewa.