TCCIA yawatambua vinara wa wasafirishaji bidhaa nje ya Tanzania

Thursday November 29 2018

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ili kuhamasisha biashara ya kimataifa, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), imewazawadia wasafirishaji maahiri wa bidhaa tofauti nchini.

Zawadi hizo zilizotolewa kwenye maadhimisho ya miongo mitatu tangu kuanzishwa kwa TCCIA, tuzo zitakazokuwa zinatolewa kila mwaka kuanzia sasa.

“Tunazo rasilimali nyingi sana nchini, kinachohitajik ani kuzitumia fursa zilizopo. Fursa haziwezi kukutafuta ni lazima uchangamke, ukijituma mafanikio yapo,” alisema Shubash Patel ambaye alikuwa mgeni rasmi wa tuzo hizo.

Patel ambaye ni mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) alisisitiza: “Tukope na kulipa kwa wakati, tukiwa waaminifu, Tanzania ya viwanda inawezekana.”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, washindi 10 walitangazwa na kupewa tuzo zao. Washindi hao walikuwa kampuni za Said Bharessa zilizoshinda kwa kuuza zaidi soko la Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Mohammed Entreprises Limited (Metl) walioongoza Afrika Mashariki.

Wakati Metl ikitunukiwa usafirishaji bora, mwenyekiti wake, Mohammed Dewji alishinda mkurugenzi bora Afrika katika tuzo za Africa Investments Forum and Awards.

Wengine walioshinda ni kampuni ya Prince Africa kinara wa kusafirisha bidhaa za pastiki nje ya nchi wakati kampuni ya Kioo ikiongoza kwa kusafirisha vifungashio na Kwanza Collections wakishamiri kwenye bidhaa za ubunifu.

Tanzania Leaf Tobacco Industries waliongoza kwenye usafirishaji wa mazao ya biashara huku kampuni ya Export Trading Group ikipata tuzo ya usafirishaji wa mazao ya chakula na Tanzania Distillers wakiongoza kwa usafirishaji wa vinywaji.

Kampuni ya Alaf ilinyakua tuzo ya usafirishaji wa vifaa vya ujenzi huku Agreko ikipata tuzo ya mwanamke aliyesafirisha zaidi.

Meneja masoko, mawasililiano na uhusiano wa Benki ya KCB ambayo ilikuwa mdhamini mkuu wa tuzo hizo, Christine Manyenye anasema: “Kwa utafiti wetu, wanawake wanarejesha zaidi kuliko wanaume hivyo tumewaandalia utaratibu maalumu. Tunawafundisha kisha wataalamu wetu wanawasaidia kurasmisha biashara zao,” anasema Christina.

TCCIA ilianzishwa mwaka 1988 na imekuwa muhimu kwa wauzaji wa bidhaa nje ya nchi. Makamu wa rais wa TCCIA, Octavian Mshiu alisema tuzo hizo zitaendelea kutolewa kila mwaka.

“Sisi ndio tunaotoa cheti cha asili ya bidhaa. Usafirishaji wa bidhaa unasaidia kuimarisha urari wa biashara na thamani ya sarafu,” anasema.


Advertisement