TCRA kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia

Thursday March 21 2019

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya Mawasiliano

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya Mawasiliano (TCRA, James Kilaba 

By Kelvin Matandiko Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imesema itaongeza kasi ya kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya teknolojia katika mifumo ya mawasiliano nchini.

Hatua hiyo inatokana na ongezeko la wananchi kutumia data zaidi katika mawasiliano ya simu ikilinganishwa na njia ya sauti.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jijini Dar es Salaam leo, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, James Kilaba amesema takwimu zinaonyesha kuna kasi kubwa ya ongezeko la matumizi ya data katika mawasiliano kuliko kupiga simu.

"Wengi wao kwa sasa wanatumia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, wanatuma meseji au kupiga, sasa ukipiga kwa kutumia WhatsApp unaikosesha Serikali mapato," amesema Kilaba alipokuwa akiwasilisha taarifa za mfumo wa kuratibu na kusimamia mawasiliano ya simu nchini (TTMS).

Changamoto nyingine wanayojipanga kukabiliana nayo ni utekelezaji wa mfumo mpya wa tozo kwa watengenezaji wa simu zikiwamo Sumsang, Huawei na  Tecno.

"Tunatambua simu zote na aina zake zinazoingizwa nchini, kwa mfano Huawei  ana simu milioni saba, zikiharibika zinakwenda wapi? kwa hiyo tutakuwa na mfumo mwingine wa ‘waste management system".

Wajumbe wa kamati hiyo wametembelea mfumo huo wa TTMS uliogharimu dola 24.6 milioni za Marekani kwa  mkataba wa miaka mitano.

Kilaba amesema mabadiliko hayo yatakuwa ni sehemu ya kuboresha mfumo wa TTMS uliozinduliwa Januari 2019 na Rais John Magufuli.

Mfumo mkuu wa TTMS katika mawasiliano nchini unajumuisha mifuko sita ambayo ni mfumo wa usimamizi wa simu za ndani na za kimataifa, mfumo wa kubaini simu za ulaghai, mfumo wa rajisi ya namba tambulishi,

mfumo wa miamala ya fedha, mfumo wa usimamizi wa ubora wa mawasiliano na mfumo wa kuhakiki mapato ya watoa huduma.

Advertisement