TCRA yazionya kampuni za simu

Muktasari:

  • Mamlaka yaMawasiliano Tanzania (TCRA)Kanda ya Kati imesema ili kukabiliana na makoa ya mtandaoni watapambana na kampuni za simu watakapobaini mtu anatumia line bila kusajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole

Dodoma.   Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kanda ya kati imesema ili kukabiliana na makosa ya mtandao watapambana na kampuni za mawasiliano ya simu nchini pindi watakapobaini mtu anatumia line bila kusajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole.

Hata hivyo, TCRA imezitaka kampuni hizo kuangalia namna ya kuzuia ujumbe mfupi wa maandishi unaotumwa namatapeli kwa watu kabla haujafika kwa wananchi.

Mkuu wa TCRA Kanda ya Kati Dodoma, Antonio Manyanda ameyasemahayo jijini Dodoma leo Jumanne Aprili 16,2019 wakati wa mkutano wa wadau wa huduma za mawasiliano mkoani humo ulioandaliwa na mamlaka hiyo kwa lengo la kujadili changamoto zilizopona kuangalia namna ya kukabaliana nazo.

“Mamlaka ya mawasiliano ilitoa namba kwa watoa huduma ili watoe huduma bora kwa wananchi, lakini inafikia hatua namba hizo zinatumika kutapeli watu na zinapitia kwenye network za kwenu hukohuko.

“Hivyo naomba mzizuie huko huko, zinaenda mpaka kutapeli watu kwani hakuna namna ya kuzizuia kabla hajaenda na kujua hawa ni tapeli?” amehoji Manyanda na kuongeza:

“Ndio maana tunasema kuanzia tarehe moja mwezi wa tano kila line ifanyiwe usajili kwa kutumia alama za vidole, tukiona line haijasajiliwa katika mfumo huo sisi tutapambana na watoa huduma kwa sababu mtakuwa mnaandaa mazingira wezeshi kufanya uhalifu,  hatutakubali.”

Akifungua mkutano huo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amewatahadharisha wote wanaojihusisha na utapeli kupitia mitandao ya mawasiliano kuwa pindi watakapokamatwa watashughulikiwa bila kigugumizi.

Mruto amesema wahalifu hao wana mtandao mkubwa hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka kutapeliwa, huku akisema wapo ambao wanatuma meseji wakitumia majina ya viongozi wakubwa ili kutapeli.