TCRA yazungumzia sauti inayodaiwa kuwa ya Nape, Kinana

Thursday July 18 2019

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba amesema mamlaka hiyo haina uwezo wa kudukua mawasiliano ya wateja wa mitandao ya simu za mkononi.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 18, 2019 baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu sauti zinazosambaa mitandaoni zikidaiwa kuwa za mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye na katibu mkuu wa zamani wa CCM, Abdulrahman Kinana wakiwa katika mazungumzo.

Kilaba amesema ni rahisi kwa mtu yeyote kusambaza sauti kama hizo, “Kusambaa hata wewe unaweza ukaanzisha tu.”

Katika sauti hiyo inayosambaa mitandaoni inasikika sauti inayodaiwa kuwa ya Kinana akimlalamikia kiongozi anayesababisha kudhalilishwa.

Sauti hizo zimeanza kusambaa mitandaoni ikiwa zimepita siku nne tangu Kinana na katibu mkuu mwingine wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba kumuandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho, Pius Msekwa  wakilalamika kudhalilishwa.

Makamba alikuwa katibu mkuu wa sita na Kinana (wa nane) walitoa taarifa ya maandishi kwa umma Julai 14, 2019 ambayo wameisaini wakimlalamikia mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Advertisement

“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo,” inasema taarifa yao hiyo.

Wastaafu hao wanasema wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu taarifa wanazodai za uzushi kwa nyakati mbili tofauti.

Walisema kwa sasa Watanzania wanajua kuwa yanayosemwa na mtu huyo si ya kwake.

Wanasema mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo, ambaye amemtaja lakini jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, anatumwa na nani?

 

Advertisement