TFDA yateketeza bidhaa za Sh20 milioni

Bidhaa mbalimbali zikiteketezwa na TFDA mjini Tabora leo. Picha na Robert Kakwesi

Tabora. Mamlaka ya Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa Tiba (TFDA), Kanda ya Magharibi imeteketeza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh20.4milioni.

Bidhaa hizo zimeteketezwa leo Jumatatu jioni katika sehemu ya kuchomea taka ya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora, Kitete.

Akizungumzia bidhaa hizo, mkaguzi wa dawa wa Kanda ya Magharibi, Frederick Luyangi amesema ni bidhaa za kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.

Amesema bidhaa hizo zilizoteketezwa ni zile ambazo hazifai na zilizoondolewa sokoni.

Alipoulizwa kuhusu wafanyabiashara waliokamatwa katika ukaguzi uliofanyika maeneo ya biashara za chakula, dawa za binadamu na mifugo, vipodozi na vifaa tiba amesema maduka matatu yamefungiwa huku wahusika wakifikishwa kwenye mkono wa sheria.

Luyangi ameomba ushirikiano wa wananchi katika kuwafichua wafanyabiashara wanaokwenda kinyume na sheria kwa kuuza bidhaa zisizofaa.

Ofisa afya mkuu wa Manispaa ya Tabora, Pachal Matagi amewaomba wafanyabiashara kuwa na huruma na wananchi kwa kutowauzia bidhaa zisizofaa.

Pia amewataka wananchi kabla ya kununua bidhaa, kuangalia muda wake wa matumizi na wanapoona muda umepita kutoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Tabora, William Mpangala amesema wanafanya utaratibu wa kupata sehemu salama ya kuteketeza bidhaa zisizofaa ambayo itakuwa nje ya mji.

Amesisitiza kuwa uteketezaji wa bidhaa zisizo salama unapaswa kufanywa pasipo kuhatarisha afya za watu na ndio maana wanatafuta sehemu nje ya mji.

Uteketezaji wa bidhaa hizo ulifanywa katika sehemu maalumu ya kuchomea uchafu unaozalishwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa Tabora, Kitete.