TFDA yatoa ufafanuzi dawa ya Menthodex inayoonyesha kutengenezwa Aprili 2019

Muktasari:

  • Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imetolea ufafanuzi kuhusu dawa ya maji ya kikohozi ya Menthodex Cough Mixture toleo namba 332W1 kuwa haijaingia kwenye mzunguko katika soko la Tanzania.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema dawa ya kikohozi ‘Menthodex’ ambayo ilionyesha kutengenezwa kiwandani Aprili mwaka huu, haijaingia kwenye mzunguko wa soko nchini.

Awali taarifa zilisambaa mtandaoni zikionyesha katika lebo ya dawa hiyo tarehe ya kutengenezwa kuwa ni Aprili 2019 na muda wa matumizi kuisha ni Aprili Mosi, 2021.

Lakini pia lebo hiyo ilionyesha kuwa dawa tajwa imesajiliwa katika nchi ya Nigeria na Mamlaka ya Dawa ya nchi hiyo (NAFDAC) kwa usajili namba 04-0971.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 22, 2019  na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Adam Fimbo imeeleza kuwa ilisajili dawa hiyo yenye ujazo wa mililita 100 na 200 kwa matumizi ya hapa nchini.

“TFDA imefanya mawasiliano na mtengenezaji wa dawa hiyo kampuni ya Bells, Sons & Company (Druggists) Limited iliyopo nchini Uingereza ambayo imekiri kwamba kulikuwa na makosa wakati wa uchapaji wa tarehe ya kutengenezwa kifungashio cha nje cha toleo la dawa hiyo,” amesema Fimbo.

Ametaja tarehe iliyostahili kuchapwa katika kifungashio hicho kuwa ni Aprili 2018 na kwamba imethibitisha kuwa toleo hilo lilizalishwa na kusambazwa katika soko la Nigeria peke yake.

“Licha ya kupata uthibitisho huo, ukaguzi uliofanywa mpaka sasa na TFDA haujabaini kuwepo kwa toleo hilo katika soko la Tanzania na matoleo mengine ya dawa hiyo yaliyopo nchini hayana mkanganyiko wa tarehe za kutengenezwa na ni salama kwa matumizi,” amesema.