TFRA yatoa dawa kwa watoto wanaumwa saratani Muhimbili

Daktari Bingwa wa watoto Mary Charles akipokea msaada wa dawa ya kutibu saratani kwa watoto kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Dk Stephene Ngailo. Dawa hiyo inagharimu Sh11.5 milioni

Muktasari:

  • Kwa siku Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatoa matibabu kwa watoto wanaumwa saratani 65 mpaka 100, hivyo mahitaji ya dawa ni makubwa.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) imetoa chupa 500 za dawa ya kutibu ugonjwa wa saratani kwa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), yenye thamani ya Sh11.5 milioni.

Akikabidhi dawa hizo leo Jumatatu Mei 6, 2019  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephane Ngailo amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha watoto wanakuwa salama.

Amesema dawa hiyo ikitibu watoto, wazazi wao watarejea nyumbani na kuendelea kushiriki shughuli  za maendeleo ikiwamo kilimo.

"TFRA tunaamini wazazi wanaouguza watoto kwa sababu ya saratani watapata ahueni watoto wao wakipona, kwa hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kutoa huduma za afya tumeleta dawa," amesema Dk Ngailo.

Akipokea dawa hizo daktari bingwa wa watoto, Dk Mary Charles amesema mahitaji ya dawa za saratani kwa watoto ni makubwa kwa sababu bei yake ipo juu.

"Chupa 500 lakini zimegharimu fedha nyingi, matibabu ya saratani ni gharama, dawa zinazotumiwa kutibu saratani ni aina moja tu hivyo uhitaji ni mkubwa," amesema.

Amesema kwa siku wanaweza kuwa na watoto kuanzia 65 mpaka 100.

"Kwa hiyo mahitaji ya dawa ni makubwa sana na ili mtoto apone anahitaji kama aina sita hivi za dawa hii ni moja tu, wengine wenye nia ya kutusaidia tunawakaribisha," amesema Dk Mary.