TLS yapata rais mpya, asikitika Lissu kupigwa risasi mchana

Rais mpya wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika(TLS ) akiapa kukitumikia chama hicho baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jijini Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jana Jumamosi kilifanya uchaguzi wa viongozi wake, ambao watakiongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja katika uchaguzi uliofanyika jijini Arusha

Arusha. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimemchagua, Dk Rugemeleza Nshala kuwa Rais wa chama hicho katika kipindi cha mwaka mmoja ujao akichukua nafasi ya Fatma Karume.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumamosi Aprili 6, 2019 ambao ulikua na ushindani mkali, Dk Nshala alipata kura 647 kati ya kura 1,217 zilizopigwa huku akiwaacha kwa mbali washindani wenzake ambao ni Godwin Ngwilimi (354), Godfrey Wasonga (123), Gasper Mwanalyela (58) na John Seka (29).

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Bahame Nyanduka alisema uchaguzi huo umezingatia kanuni, sheria na taratibu wa chama hicho ambacho kina jukumu la kusimamia uongozi wa sheria unatamalaki.

Katika nafasi ya makamu mwenyekiti alichaguliwa, Mpale Mpoki, nafasi ya Mweka Hazina, Nicholaus Duhia huku nafasi za wajumbe wa baraza la uongozi ni Angelista Nashon, Tike Mwambipile, Paul Kaunda, Jebra Kambole, Harold Sungusia, Baraka Mbwilo na Stephen Mwakibolwa.

Dk Nshala katika hotuba yake ya shukrani alisema atatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na anaamini kila mwanachama atamuunga mkono kutekeleza majukumu yake.

Alisema inasikitisha kuona aliyekua Rais wa TLS, Tundu Lissu alipigwa risasi mchana kweupe lakini hakuna mtu hata mmoja ambaye amekamatwa na kuchukuliwa hatua jambo ambalo linatia shaka utawala wa sheria.

Lissu alipigwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7, 2017 jijini Dodoma na tangu siku hiyo yupo nje ya nchi akipatiwa matibabu zaidi.