TMA: Kimbunga Kenneth kipo kilomita 600 kutoka Pwani ya Tanzania

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), Dk Pascal  Waniha akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati akitoa taarifa ya mrejeo wa mwenendo wa mgandamizo mdogo wa hewa uliopewa jina la ''Kenneth'' katika bahari ya Hindi na athari zake kwa maeneo mbalimbali hapa nchini. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

TMA imesema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kimbunga Kenneth kilichopo eneo la Kaskazini Magharibi mwa Kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mgandamizo wa hali ya hewa umefikia katika hatua ya kimbunga halisi chenye ukubwa wa mwendokasi wa upepo unaozunguka kilomita 160 kwa saa.

TMA ambayo ilikitambulisha kimbunga hicho kwa jina la Kenneth, imesema kufikia saa 3:00 asubuhi leo Jumatano Aprili 24, 2019 kimefikia hatua ya sita na kipo kilomita 600 kutoka Pwani mwa Tanzania na Msumbiji.

 

Akizungumza katika mkutano wa vyombo vya habari leo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA, Dk Pascal Waniha, amesema asubuhi ya leo kimbunga hicho kimeonekana katika visiwa vya Commoro kikitembea kwa kasi ya kilomita 150 kwa mzunguko.

“Usiku kitasogea zaidi kufikia umbali wa kilomita 250 kwa mzunguko wa kasi ya juu ya upepo wa kilomita 150 kwa saa,” amesema Dk Waniha.

Amesema wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka TMA na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake.

Dk Waniha amesema TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa kimbunga hicho Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi.