TMA yatoa angalizo mvua zenye athari

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetangaza utabiri wa hali ya hewa wa siku tano kuanzia Aprili 23 hadi 26 mwaka huu na kutoa angalizo la uwepo wa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa angalizo la uwepo wa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi, zitakazoacha athari katika shughuli za, kijamii, kiuchumi, uvuvi na usafiri baharini, pamoja na baadhi ya makazi kuzingirwa na maji.

Mikoa iliyotajwa kukumbwa na hali hiyo ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa TMA, Samwel Mbuya ameiambia Mwananchi leo Aprili 22, 2019 kuwa wananchi wanatakiwa kujiandaa kwani kutakuwa na mawimbi makali, upepo mkali na mvua kubwa.

Ametaja athari hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema kutakuwa na kutawanyishwa/kupeperushwa kwa takataka mitaani, kuanguka kwa majani na matawi madogomadogo ya miti, kuathirika kwa baadhi ya shughuli za uvuvi na usafiri baharini pamoja na ugumu wa upatikanaji wa samaki.