TPSF yachungulia fursa mradi wa umeme Rufiji

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye

Muktasari:

  • Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema mkutano huo utafanyika Juni 11.

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura) itawakutanisha wadau kujadili fursa zilizopo kwenye mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji.

Lengo la kukutanisha wadau ni kufanya upembuzi na uchambuzi wa fursa zilizopo kwenye mradi huo ambazo wafanyabiashara wazawa wanatakiwa kuzichangamkia.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema mkutano huo utafanyika Juni 11.

Alisema mkutano huo utaongeza uelewa wa wadau kwenye mradi huo na fursa zilizopo na miongoni mwa watakaohudhuria ni makandarasi kutoka nchini Misri wanaotekeleza mradi huo na Tanesco.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NEEC, Bengi Issa alisema katika mradi huo wanategemea ushiriki wa Watanzania katika maeneo yote.

Alisema kwamba mkandarasi atakayetekeleza anapaswa kutoa mpango na atatenga ajira kiasi gani kwa Watanzania na maeneo gani ikiwamo mafunzo ya utaalamu.