TPSF yapigia chapuo ubia wa kibiashara na Afrika Kusini

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPFS), Salum Shamte

Muktasari:

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPFS), Salum Shamte amemwambia Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa kuchochea ubia wa kibiashara miongoni mwa sekta binafsi za Tanzania na Afrika Kusini kwa kuwa mazingira ya sasa Tanzania yanavutia kibiashara na tayari kero mbalimbali za kibiashara zimeshapata suluhisho.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPFS), Salum Shamte amepigia chapuo la kuhamasisha mazingira ya ubia wa kibiashara kati ya wajasirimali wa Tanzania na Afrika Kusini.

Shamte amemwambia Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kuwa mazingira ya sasa Tanzania yanavutia kibiashara na tayari kero mbalimbali za mazingira ya kibiashara zimeshapata suluhisho baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango wa kushughulikia vikwazo vya kibiashara wa ‘Blueprint’.

Kwa mujibu wa TPFS, taasisi hiyo inayounganisha mtanda wa wafanyabiashara takribani milioni 4.5, unahusisha asilimia 98 ya utegemezi katika soko la ajira.

“Tunatambua uwezo wa kiteknolojia, kimitaji na kibiashara katika sekta mbalimbali, tunaamini kwamba kwa kufanya kazi pamoja kupitia ubia, tutaweza kufikia mafanikio makubwa yatakayokuwa na manufaa kwa pande mbili,” amesema Shamte ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Biashara linalohusisha taasisi za Sekta binafsi katika Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC).

Shamte ametoa kauli leo Alhamisi Agosti 15, 2019 wakati wa Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Rais Ramaphosa aliyeingia nchini Tanzania jana Jumatano kwa ziara ya siku tatu kabla ya kushiriki Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi 16 za SADC.

“Tunaomba, kila uwekezaji utakaofanyika ni vyema ukazingatia mazingira ya ubia kwa wajasiriamali wadogo ili kuhakikisha manufaa kwa pande zote, ujio wako kupitia ziara hii Tanzania umejitokeza kwa wakati muafaka kuona mazingira shawishi ya uwekezaji tuliyonayo, itasaidia kuimarisha zaidi mahusiano ya kibiashara kati yetu,” amesema Shamte.

“Tunawakaribisha sana watu kutoka Afrika kusini kwa ajili ya ubia na Watanzania kuwekeza katika mazingira ya manufaa ya pande zote,” ameongeza